Kukosekana mvua kwa misimu minne mfululizo katika maeneo ya Ethiopia, Kenya na Somalia kunatishia kutokea baa la njaa katika jumuiya za pembe ya Afrika.
Hali hii haijawahi kushuhudiwa katika miaka 40 iliyopita ambapo mvua za chini ya wastani zimefanya maeneo ya Somalia, kusini na kusini mashariki mwa Ethiopia, na kaskazini na mashariki mwa Kenya kukabiliwa na ukame ambao umeongeza hatua za watu kuhama.
Kwa mujibu wa shirika la misaada takriban mifugo milioni 7 imekufa kote katika ukanda huo.
Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa – UNICEF – linasema zaidi ya watoto milioni 7 wanakabiliwa na kudumaa kutokana na kukosa lishe bora.