Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 04:48

Somalia inasema ina utajiri wa kutosha kuinufaisha Jumuiya ya Afrika Mashariki


Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud katika mahojiano na shirika la habari la Reuters katika ikulu rais mjini Mogadishu, Somalia, May 28, 2022. Picha: Reuters
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud katika mahojiano na shirika la habari la Reuters katika ikulu rais mjini Mogadishu, Somalia, May 28, 2022. Picha: Reuters

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amewaomba viongozi wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kukubali maombi ya Somalia kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo.

Rais Mohamud ameambia kikao cha marais wa Jumuiya ya Afrika mashariki mjini Arusha, Tanzania kwamba Somalia ilituma maombi ya kuwa mwanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2014 lakini mazingira yaliyokuwepo wakati huo hayakuruhusu maombi hayo kushughulikiwa.

Nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki zilikataa maombi ya Somalia kutokana na ukosefu wa usalama katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa nchi ya hivi karibuni (Julai 11, 2022) kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo kuongeza mapato ya ndani katika jumuiya hiyo kwa asilimia 22.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema hivi karibuni kwamba watu katika jumuiya ya Afrika Mashariki wameanza kufurahia makubaliano ya kusafiri kutoka nchi moja hadi nyingine bila vizuizi. Usafiri wa bidhaa vile vile umerahisishwa.

Ukosefu wa usalama Somalia

Somalia imekuwa ikikabiliana na ukosefu wa usalama kwa miongo kadhaa na rais aliyeondoka Mohamed Abdullahi maarufu kama Farmaajo, ameshutumiwa kwa kile kimetajwa kama kutoonyesha nia ya dhati kutaka Somalia kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais wa sasa Mohamud, amesema kwamba “Somalia imekuwa na kiu ya muda mrefu ya kutaka kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na uhusiano wake wa kitamaduni, kihistoria, lugha na kiuchumi na nchi za Afrika Mashariki.”

Mojawapo ya kanuni kwa nchi inayotaka kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuwa na utawala bora, kuheshimu demokrasia, mfumo wa sheria na kuweko haki kwa wote.

Kila nchi mwanachama inastahili kuchangia katika kukuza jumuiya hiyo.

Utajiri wa Somalia

Somalia ina jumla ya watu milioni 16 lakini idadi kubwa ya wasomali wanaishi katika nchi nyingine za Afrika Mashariki hasa Kenya na pia nje ya bara la Afrika.

Nchi hiyo ina raslimali nyingi ikiwemo madini ya uranium, chuma, shaba, chumvi na gesi asilia.

Somalia pia imetoa leseni kwa kampuni za Australia na China kubaini iwapo ina mafuta.

Ina zaidi ya ekari milioni 8 zenye rotuba ya juu kwa ajili ya kilimo, pamoja na pwani yenye urefu wa kilomita 3,000, ikiwa ndiyo pwani kubwa zaidi Afrika na yenye utajiri mkubwa wa samaki na shughuli za utalii.

Nchi hiyo ina kiasi kikubwa cha dhahabu kinachoifanya kuwa ya pili kwa utajiri wa dhahabu Afrika.

Japo rais wa Somalia Mohamud amesema kwamba nchi yake ina hali ya utulivu, inaendelea kukabiliwa na mashambulizi kutoka kwa kundi la kigadi la Al-shabaab.

Wafanyabiashara wa Somalia wamefanikiwa kibiashara

Raia wa Somalia ni wafanyabiashara wakubwa hasa Kenya na Dubai. Wafanyabiashara kutoka Somalia wanatajwa kuwa mojawapo ya wafanyabiashara wakubwa Dubai baada ya wafanyabiashara kutoka Iran.

Nchini Kenya, wafanyabiashara kutoka Somalia wanashindana sana na wale kutoka India hasa katika biashara ya vyombo vya mawasiliano, nguo, kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu, usafiri na hata katika kuuza nyumba au ardhi.

Wasomali pia wanafanya sana biashara Mashariki ya Kati, Afrika Kusini, Tanzania, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Afrika ya Kati.

“Tunataka kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu watu wetu wapo kila mahali katika eneo hili,” amesema rais Mohamud.

Faida ya Somalia kujiungana jumuiya ya Afrika mashariki

Iwapo Somalia itajumuishwa katika jumuiya ya Afrika Mashariki, idadi ya watu katika jumuiya hiyo itaongezeka hadi milioni 300 na hivyo kuongeza ukubwa wa soko hilo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ina nchi 7 ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

XS
SM
MD
LG