Lakini wanapoondoka ofisini, tume hiyo inasalia bila kamishna yeyote kufuatia kufukuzwa kwa makamishna wengine wanne baada ya kupinga kutangazwa kwa William Ruto kuwa mshindi wa kura ya urais ya Agosti 9, mwaka 2022.
Chebukati anaondoka ofisini baada ya kuhudumu kwa muhula mmoja wa miaka sita kwenye tume hiyo ya uchaguzi nchini Kenya pamoja na makamishna wengine wawili—Boya Molu na Prof Abdi Guliye—na kudai kufanikisha mageuzi makubwa kwenye tume hiyo, na kujivunia kufanya kazi vizuri licha ya kuwepo shinikizo la awali kufurushwa. Lakini raia wa Kenya nao wana hisia tofauti kuhusu utendakazi wake. Wapo wanaopongeza utendakazi wake licha ya kuwapo na shinikizo la kisiasa.
Pia wapo wanaomshtumu alivyoendesha shughuli za tume kwa maslahi ya umma.
Ahmed Issack Hassan
Chebukati ambaye aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa tume hiyo mnamo Januari 18, 2017 na kumrithi Ahmed Issack Hassan na makamishna tisa walioondoka ofisini mapema baada ya kupata malipo ya kuachishwa kazi, na kumaliza shinikizo na mzozo wa siku nyingi wa kisiasa uliokuwa umetokota nchini Kenya kuhusu kuendelea kuhudumu kwao.
Licha ya kuwa ofisini muda huo wote, Chebukati amepitia shinikizo la kisiasa kila wakati uchaguzi mkuu unapokaribia. Hata anapoeleza kuwa anaona ni fahari kuwahi kuhudumu kwenye wadhifa huo, amejikuta kwenye tume ambayo kila wakati wa uchaguzi mkuu inaingiliwa na kusambaratishwa na madai ya uingiliaji wa maslahi ya kisiasa.
Uchaguzi wa 2017
Katika uchaguzi wa 2017 IEBC ilimtangaza Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa kura ya urais na baadaye kubatilishwa na mahakama ya juu iliyoongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wakati huo David Maraga.
Nusu ya makamishna wa tume hiyo wanaowajumuisha Consolata Nkatha Maina, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya walijiuzulu kwa kutaja uongozi wake kuwa usioridhisha na kukosa imani naye na vile vile madai ya tume kuingiliwa na watu wa nje.
Kamishna Roselyn Akombe alijiuzulu awali siku chache kabla ya marudio ya kura ya urais, aliyefanya hivyo kutokana na madai kuwa tume hiyo ilikuwa imetekwa na maslahi ya kisiasa.
Mwaka 2022, wakati wa uchaguzi mkuu, Bw Chebukati vile vile alijikuta chini ya shinikizo hilo baada ya makamishna wanne wa tume hiyo kuibeza hatua yake ya kumtangaza mgombea wa urais William Ruto kuwa mshindi wa kura hiyo.
Juliana Cherera
Aliyekuwa naibu mwenyekiti wa tume hiyo Juliana Cherera pamoja na waliokuwa makamishna wa tume hiyo Francis Wanderi, Justus Nyang’aya na kamishna aliyesita kujiuzulu na kufikishwa mbele ya jopo linalowachunguza wanne hao, Irene Masit.
Kwa kauli moja walimtaja Chebukati kuwa msiri mno na kwamba aligomea jitihada za kuwahusisha katika awamu ya mwisho ya uthibitishaji wa matokeo ya urais jinsi yalivyonakiliwa kwenye fomu 34B zinazohifadhi matokeo ya kura ya urais kutoka kwa maeneo bunge 290. Na hawangeweza kujihusisha na tangazo la Ruto kuwa mshindi.
Japo alikanusha madai hayo na kuwataja wanne hao kuwa na nia ya kutekeleza kwa siri jaribio linalofananishwa na kufanyika kwa mapinduzi kwa kushinikiza na kulazimisha iandaliwe duru ya pili ya uchaguzi huo, wafuatiliaji wa siasa za Kenya wanalitaja hilo kuwa doa kwenye utendakazi wake.
Mchakato wa Kujaza Nafasi IEBC
Mchakato wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi unatarajiwa kuchukua muda zaidi kando na ilivyotarajiwa kwani jopo linalochunguza wanne hao linaendelea na vikao vyake na mapendekezo yake bado hayajawasilishwa kwa rais kwa utekelezaji.
Pia, mswaada unaolenga kufanyia marekebisho sheria ya IEBC ili kubadilisha muundo wa jopo la uteuzi linalosimamia kujaza nafasi zilizoachwa wazi katika tume hiyo, ungali kwenye bunge la Seneti ambalo kwa sasa lipo kwenye likizo hadi Februari.
Hata hivyo, Chebukati anapoondoka, anapendekeza rais Ruto kuchunguza vurugu zilizotokea katika ukumbi wa Bomas alikotangazwa mshindi wa kura ya urais. Pia, anapendekeza kuteuliwa kwa makamishna wapya angalau miaka miwili kabla ya Uchaguzi Mkuu. Vile vile anatoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano na Bunge kuharakisha marekebisho ya sheria za uchaguzi kwa wakati unaofaa kabla ya uchaguzi.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya.