Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:49

Mawakili wa Odinga na IEBC wajibizana kuhusu raia wa Venezuela


Kikao cha mahakama ya Kenya inayosikiliza kesi ya kupinga ushindi wa rais mteule Dr. William Ruto.
Kikao cha mahakama ya Kenya inayosikiliza kesi ya kupinga ushindi wa rais mteule Dr. William Ruto.

Majibizano makali yalitokea mahakamani kati ya wakili wa Raila Odinga na wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kuhusu madai kwamba mojawapo ya fomu iliyokuwa kwenye mfumo wa digitali wa tume ya uchaguzi, ilikuwa na ‘ushahidi kwamba raia wa Venezuela alidukuwa mfumo wa IEBC.’

Wakili James Orengo, anayeongoza timu ya mawakili ya Raila Odinga, alikuwa anajaribu kumzuia wakili wa IEBC Prof Githu Muigai, kuieleza mahakama kwamba fomu iliyowasilishwa na timu ya Odinga, na namna ilivyowasilishwa, ilikuwa na lengo la ‘kuipotosha mahakama.’

Wakati wa kikao cha Ijumaa asubuhi, wakili wa Odinga, Julie Soweto, aliionyesha mahakama fomu 34A kutoka kituo cha kupigia kura cha shule ya msingi ya Gacharaigo, Kaunti ya Murang’a, iliyokuwa na jina la raia wa Venezuela Jose Camargo.

“Mahakama imetaka tuonyeshe ushahidi, kwa kutumia mifano sahihi, namna fomu 34A ilivyodukuliwa au inavyoweza kudukuliwa.” Ameanza kueleza wakili Soweto, akiiomba mahakama kufanya hivyo kwa kuonyesha kwenye video mahakamani, akipakua fomu 34A kutoka kwa wavuti wa IEBC. Kimya kilitanda mahakamani, kila mtu akimsikiliza Soweto na macho yote kwenye ukuta uliokuwa unaonyesha video yake.

“Naona kwamba karibu kila mtu hapa mahakamani ana tarakilishi na anaweza kuingia kwa mfumo wa digitali wa IEBC na kupakua hii fomu mwenyewe. Naenda kuwaonyesha mambo haya moja kwa moja namna mahakama imetaka tufanye.” Ameendelea kusema wakili Soweto, akisistiza kwamba “tumeshutumiwa kwa kusema uongo, kuwasilisha nyaraka ghushi. Tumeshutumiwa na kutajwa kuwa watu waongo.”

Wakili Soweto amekielezaHkikao cha mahakama na kuonyesha fomu ambayo upande wa juu, kushoto, ulikuwa na jina la Jose Camargo. “haya ninayowaonyesha ni ya moja kwa moja. Nataka mahakama kuangalia na kuhakiki hii fomu kabla ya kufanya jambo lingine lolote.”

Amesema kwamba ‘idadi ya kura kwenye fomu hii imebadilishwa. Idadi imeongezwa. Tumeambiwa kwamba hakuna raia wa kigeni aliingia kwenye mfumo wa IEBC. Hili jina la Camargo lilifikaje huku. Tumekuwa tukitafuta ushahidi. Kwa upendo wa mungu, tumepata. Tumetaka kuwaonyesha moja kwa moja, na tunawaonyesha moja kwa moja kutoka kwa mfumo wa IEBC.”

Mawakili wa IEBC na wa Ruto waomba kujibu shutuma

Mawakili wa rais mteule William Ruto na wa tume ya uchaguzi, waliomba mahakama mara kadhaa wakitaka kujibu shutuma hizo, lakini maombi yao yalionekana kukataliwa.

Mawakili wa Odinga walipinga maombi ya kutaka mawakili wa IEBC kujibu shutuma hizo.

Saa kadhaa baadaye, wakili wa William Ruto aliomba jaji mkuu kwamba ilikuwa muhimu kwao kujibu shutuma zilizokuwa zimetolewa kwa sababu zilikuwa zimeenea kote nchini kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Wakili wa Ruto Fred Ngatia, aliomba jaji mkuu kuasilisha ushahidi waliokuwa nao, kwa kuzingatia kwamba 'mawakili wa Odinga walikuwa wameasilisha ushahidi mpya na ni vyema wakipewa nafasi ya kujibu".

"Tutajadiliana kati yetu (majaji) halafu tutafanya uamuzi iwapo tutakubaliana kama ulikuwa ushahidi mpya", amesema jaji mkuu Martha Koome.

Mawakili wa IEBC na Ruto wapewa nafasi ya kujibu

Wakili wa IEBC Mahat Somane alianza ushahidi wake kwa kusema kwamba “ningependa kujibu maswali matatu ambayo yamesemwa hapa mahakamani na wakili mwenzangu Julie Soweto. La kwanza linahusu fomu ambayo ameonyesha hii mahakama. Ningependa hiyo fomu ionyeshwe kwa njia ya video kwa hii mahakama. Hiyo fomu ambayo wakili Julie ameionyesha mahakama ndio nataka kuionyesha mahakama. Nataka kuipa mahakama fomu halali 34A ya hiyo inayoonekana kwenye video.”

Wakili wa IEBC, ameieleza mahakama kwamba Jose Carmago ni jina la afisa wa kampuni ya Smartmatic ambayo ilipewa kazi ya kusimamia mfumo wa digitali wa IEBC.

Kulingana na maelezo ya IEBC, jina hilo lilitokea kwenye picha ambayo wakili wa Odinga alikuwa akionyesha kwa sababu fomu 34A iliwekwa juu ya karatasi jingine lililokuwa na jina la Jose, na picha kuchukuliwa na wala halina uhusiano wowote na fomu 34A.

IEBC imeeleza kwamba jina Jose Carmago linapatikana katika karatsi nyingi sana za tume hiyo ikiwemo bahasha kwa sababu ni mfanyakazi wa Smartmatic international. Na kwamba picha hiyo yenye jina Jose Carmago, ilikuwa ya usajili.

Fomu halisi 34A iliyowasilishwa na IEBC mahakamani, na iliyosainiwa na mawakala wa wagombea wote wa urais, haina jina hilo.

Wakili wa Odinga walijaribu kuzuia IEBC kutoa Ushahidi

Wakili wa Raila Odinga, James Orengo alijaribu kumzuia wakili wa IEBC kuionyesha mahakama ushahidi waliokuwa nao kwamba ‘wakili wa Odinga walikuwa wameiambia mahakama uongo kuhusu jina la Jose Carmago kwenye fomu 34A.’

Orengo alisema kwamba wakili Mahat alikuwa anajaribu kuleta ushahidi upya bila kuwa na shahidi na kwamba mahakama haiwezi kumruhusu kuwasilisha aliyokuwa nayo.

‘Tunachofanya ni kuingia dunia nyingine ambapo Mahat analeta ushahidi upya na huko anakokwenda ni hatari sana. Iwapo anaendelea hivyo, itakuwa vigumu kuendelea na kikao hiki.”

Lakini wakili anayeongoza tume ya uchaguzi IEBC Prof Githu Muigai, alikuwa mwepesi wa kusimama na kumjibu Orengo.

“Tunachojaribu kufanya ni kuonyesha mahakama Ushahidi ambao tayari tuliwasilisha kwa mahakama. Tunatumia ushahidi huo kujibu yale ambayo wenzetu wamewasilisha mbele ya mahakama hii. Nyaraka walizotumia hazikuwasilishwa kwa mahakama wakati walipokuwa wanawasilisha kesi. Tunapotaka kuonyesha kwamba kuna nia ya dhati ya kusema uongo, wanajaribu kutuzuia kabisa. Hili ni jaribio la kutaka kuzuia ukweli usijulikane.”

Jaji Mkuu Martha Koome aliingilia kati na kuiruhusu IEBC kutoa ushahidi wake.

XS
SM
MD
LG