Hafla ya uapisho itafanyika katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Kasarani, nje kidogo ya mji mkuu, Nairobi.
Kwa mujibu wa katiba ya Kenya, rais mtele ni lazima aapishwe kati ya Saa nne asubuhi na saa nane mchana.
Mahakama ya juu ya Kenya iliamuru Jumatatu wiki jana kwamba Ruto alimshinda mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga, katika uchaguzi wa urais uliofanyika tarehe tisa mwezi Agosti, baada ya Odinga kupinga matokeo yaliyokuwa yametangazwa na tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC.
Jumatatu, Ruto alikutana na rais anayeondoka Uhuru Kenyatta kwenye ikulu mjini nairobi, huku mchakato wa kukabidhiana mamlaka, ulioanza Jumanne wiki jana ukiendelea.
"Tumekamilisha matayarisho ya hafla hiyo na ni matumaini yetu kwamba itafanyika kwa amani," alisema kaimu mwenyekiti wa tume ya ukabidhianaji madaraka, Karanja Kibicho, akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu mjini Nairobi.
Rais Uhuru Kenyatta, ambaye awali hakuwa amempongeza naibu wake William Ruto moja kwa moja kwa ushindi wake, alitoa pongezi katika hotuba yake na kumtakia kila la heri kama kiongozi ajaye wa nchi hiyo.
Darzeni za viongozi wa nchi na serikali wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo.
Tunatarajia takriban watu 60,000 kuhudhuria hafla hiyo, wakiwemo viongozi wa nchi na serikali waptao 20 kutoka sehemu mbalimbali. Tuko tayari kabisa," alisema Kibicho.
Wakati huo huo, Odinga ambaye hajazungumza moja kwa moja na Ruto tangu mahakama kutoa uamuzi wake, amesema hatahudhuria hafla hiyo ya uapisho.
Odinga alisema yuko nje ya nchi, na kwamba ana mashaka mengine. Katika taarifa, mwanasiasa huyo mkongwe alikiri kwamba alikuwa amepokea mwaliko.
Alichukua fursa hiyo kuinyooshea kidole Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa "kutotenda haki katika kuendesha uchaguzi huo."
Alisema ingawa yeye na muungano wa kisiasa aliouwakilisha waliheshimu uamuzi wa mahakama ya juu, hawakukubaliana na jinsi ilivyoshughulikia kesi hiyo.