Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 17:35

Raila Odinga kuanza tena mchakato wa kurekebisha katiba Kenya


Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akihutubia waandishi wa habari baada ya kutangazwa matokeo ya kura za urais Aug 16,2022.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga akihutubia waandishi wa habari baada ya kutangazwa matokeo ya kura za urais Aug 16,2022.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga, amesema kwamba timu yake inapanga kuanzisha tena mchakato wa kufanyia marekebisho katiba ya nchi hiyo, akisistiza kwamba mapendekezo hayo yatakuwa mapana na kuhusisha maoni ya wakenya.

Katika mahojiano na runinga ya Citizen, Odinga amesema kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa na rais wa nchi hiyo Dkt. William Ruto, kuanzisha ofisi ya mpinzani mkuu wa serikali hayastahili, na kwamba raia wa Kenya ndio wanaostahili kufanya maamuzi ya mwisho kuhusu katiba.

Odinga ameendelea kudai kwamba alishinda uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2022, lakini matokeo ya uchaguzi huo yalifanyiwa ukarabati katika kituo cha kitaifa cha kujumulisha matokeo ya kura za urais, katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Odinga ameeleza kuwa mapendekezo ya katiba yaliyowasilishwa kupitia mfumo wa maridhiano ya kisiasa kati yake na rais mstaafu Uhuru Kenyatta, yanahitajika sasa ili kuponya makovu ya ghasia za uchaguzi, ukabila, chuki, ufisadi na kujumulisha wakenya wote serikalini.

Amesema kwamba mchakato huo, utaanza Januari mwaka ujao, na masuala yote ambayo hayakujumulishwa katika harakati za awali ambazo zilidhibitiwa na mahakama ya juu, maarufu BBI, yatajumulishwa na kutoa fursa kwa raia wa Kenya kufanya uamuzi wa kutosha kuhusu mustakabali wa nchi yao.

“Tutaanzisha mchakato wa marekebisho ya katiba ambayo yatashirikisha kila mtu. Katiba imemaliza miaka 12 na inahitaji kufanyiwa marekebisho kwa sababu sasa tunajua pale kuna makosa yanayohitaji kurekebishwa,” amesema Odinga.

Mapendekezo ya rais William Ruto ambayo Odinga anapinga

Rais William Ruto, kupitia kwa bunge la Kenya, amependekeza kubuniwa kwa ofisi rasmi ya Kiongozi wa Upinzani nchini Kenya.

Amependekeza mabadiliko ya kisheria ili kuwezesha Kiongozi wa upinzani kuwa na mamlaka ya kisheria kutathmini utendakazi wa serikali.

Kulingana na sheria inayopendekezwa, muda wa uongozi wa kiongozi wa upinzani na naibu wake utaanza tarehe ambayo rais mpya anaapishwa na kumalizika wakati rais mpya anachaguliwa.

Kiongozi rasmi wa Upinzani atadhibitiwa dhidi ya aina yote ya kesi za jinai au madai katika kipindi cha uongozi, lakini anaweza kuondolewa ofisini kupitia hoja ya kutokuwa na imani naye, kupitia bungeni.

Kiongozi wa Upinzani, atakuwa na nguvu za kuchunguza, kutathmini, kukosoa na kutoa mapendekezo ya maboresho ya sheria, sera na mapendekezo ya kifedha ya serikali, kuchunguza matumizi ya fedha za umma, kutathmini, kukosoa na kuiwajibisha serikali.

Atakuwa pia na uwezo wa kuhutubia kikao maalum cha Bunge mara moja kila mwaka au wakati wowote anapohiari kufanya hivyo.

Kiongozi rasmi wa upinzani atakuwa mgombea aliyependekezwa na chama cha kisiasa au chama cha muungano au muungano wa vyama vya kisiasa ambavyo vilipata idadi kubwa ya pili ya kura katika uchaguzi mkuu.

Chama (au muungano wa vyama) kitakachomteua mpinzani mkuu wa serikali kitahitajika kupata angalau asilimia 25 ya viti katika bunge la kitaifa.

Mapendekezo hayo yanatarajiwa kujadiliwa bungeni Februari mwaka ujao 2023.

Majaji wa mahakama kuu nchini Kenya wakiwa katika kikao jijini Nairobi, Kenya wakati wa kuamua kuhusu kesi ya kupinga marekebisho ya katiba ya Kenya BBI, March 31, 2022
Majaji wa mahakama kuu nchini Kenya wakiwa katika kikao jijini Nairobi, Kenya wakati wa kuamua kuhusu kesi ya kupinga marekebisho ya katiba ya Kenya BBI, March 31, 2022

Mapendekezo yaliyopingwa na mahakama ambayo Odinga alikuwa anaunga mkono

Mapendekezo ya kufanyia marekebisho katiba maarufu BBI, ambayo yaliongozwa na rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Raila Odinga yalijumulishwa yafuatayo;

  • Kubuniwa nafasi ya waziri mkuu na manaibu wawili
  • Mawaziri na manaibu wake wanaoweza kuteuliwa kutoka bunge
  • Kiongozi rasmi wa Upinzani
  • Kuwapo kwa maeneo bunge mapya 70 hasa katika eneo la mlima Kenya
  • Kuwapo wabunge 360 wote wanaochaguliwa na wapiga kura, kutoka maeneo bunge 290 ilivyo sasa
  • Maseneta 94 waliochaguliwa na wananchi.
  • Kila jimbo kuchagua Seneta mmoja wa kike na mmoja wa kiume ili kuwepo usawa wa kijinsia.
  • Vijana kupewa msamaha wa kutolipa ushuru kwa muda wa miaka 7
  • Vijana waliochukua mkopo wa serikali kwa ajili ya elimu kuanza kulipa miaka 4 baada ya kumaliza masomo yao

Mbona Odinga anapinga mapendekezo ya Ruto?

Kulingana na Odinga, ambaye ni kiongozi wa chama cha Orange democratic movement ODM, kilicho katika muungano wa Azimio, mapendekezo yaliyowasilishwa na rais Ruto hayazingatii namna mahakama ilivyoamuru wakati ilipotupilia mbali BBI kwamba lazima raia washiriki vikamilifu katika mchakato huo.

“Mapendekezo yetu yalikataliwa na hawa watu wanaoleta mapendekezo yao sasa… walikataa mapendekezo hayo na sasa wanayaleta kupitia mlango wa nyuma,” amesema Odinga.

Kuna tofauti kubwa kati ya mapendekezo ya rais Ruto na yale yakiyokataliwa na mahakama, yaliyokuwa yanaungwa mkono na Raila Odinga.

Kwa mfano, hakuna nafasi ya waziri mkuu na manaibu wake katika mapendekezo yaliyo bungeni kwa sasa.

Odinga aliwahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa iliyoundwa baada ya ghasia za uchaguzi mkuu mwaka 2007. Alikuwa waziri mkuu wakati Mwai kibaki akiwa rais.

Matokeo ya urais katika uchaguzi wa Agosti 2022

Odinga vile vile hajakubali kwamba alishindwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka 2022, licha ya mahakama kutupilia mbali kesi yake ya kupinga matokeo hayo.

Kesi hiyo ilitupiliwa mbali kwa kukosa uchaguzi. majaji wote walikubaliana kwamba haikuwa na ushahidi licha ya Odinga na mawakili wake kusisitiza kwamba walikuwa na ushahidi wa kutosha.

Amesema kwamba tume huru ya uchaguzi IEBC ilimnyima ushindi na kumtangaza William Ruto kuwa mshindi.

Kulingana na Odinga, muungano wake wa Azimio ulikuwa na mawakala wa kutosha katika kila kituo cha kupigia kura, akifutilia mbali ripoti kwamba hakuwa na waakilishi katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.

“Kwa mara ya kwanza, wakenya walishuhudia tume ya uchaguzi iliyogawanyika. Makaminsha 4 walikataa matokeo na 3 wakaidhinsiha matokeo hayo. Hii ina maana kwamba idadi kubwa ya makamishna walikataa matokeo hayo. Ni jambo la kusikitisha kwamba mwenyekiti wa tume ya uchaguzi aliamua kutangaza matokeo hayo.”

Odinga anataka ukaguzi wa kina wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa urais kufanyika ili kuwezesha wapiga kura kuwa na imani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Makamishna 4 wa IEBC walioakataa matokeo ya uchaguzi wa urais wakiongozwa na naibu mwenyekiti Jualiana Cherera (anayehutubia waandishi wa habari) Agosti 15, 2022
Makamishna 4 wa IEBC walioakataa matokeo ya uchaguzi wa urais wakiongozwa na naibu mwenyekiti Jualiana Cherera (anayehutubia waandishi wa habari) Agosti 15, 2022

Makamishan 4 wa IEBC waliopinga matokeo wanachunguzwa

Tume maalum imeundwa kuchunguza mwenendo wa makamishna 4 wa tume huru ya uchaguzi ya Kenya IEBC wakati wa kutangaza matokeo ya kura za urais.

Ushahidi uliotolewa kufikia sasa 'unaonyesha' kwamba makamishna hao walikuwa wakiwasiliana na maafisa wa ngazi ya juu katika muungano wa Azimio, wake Raila Odinga, akiwemo Raphael Tuju na katibu mkuu wa chama cha Kenya African National union - KANU, Nick Salat.

Tume hiyo vile vile imeambiwa kwamba makamishna hao walikuwa wamelipiwa hoteli, ambapo walikuwa wakiishi na kuwasiliana na viongozi wa Azimio.

Walilipiwa pia hoteli na kuandaliwa kikao na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena jijini Nairobi kukataa matokeo ya uchaguzi ambayo yalikuwa yanatangazwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC.

Vikao vya tume hiyo ya uchunguzi vitaendelea mwaka ujao 2023.

Mwandishi wetu wa Nairobi Kennedy Wandera amechangia kuandika ripoti hii.

XS
SM
MD
LG