Kiongozi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Dennis Francis amewaambia viongozi ambao wanahudhuria mkutano wa 19 wa NAM jijini Kampala kwamba anasikitishwa na maafa yanayoongezeka huko Ukanda wa Gaza na kutaka vita kati ya Israel na Hamas visitishwe.
Katika hotuba yake kwenye kongamano hilo la wakuu wa nchi na serikali, Francis alitoa wito kwa Vuguvugu hilo kutumia ushawishi wake na kukomesha mauaji yanayoshuhudiwa kila siku katika Ukanda wa Gaza.
“Nitaunga mkono na kuhimiza mipango yoyote ya kuleta usalama na kutetea haki za binadamu’ pia, natoa wito kwa viongozi wa Vuguvugu hili kuonyesha ushawishi wao katika kukomesha mauaji ambayo tunashuhudia katika ukanda wa Gaza’’ Francis alisema.
Katika halfa hiyo, Umoja wa Afrika pia ulilaani mashambulizi ya kijeshi yanayotekelezwa na Israel huko Gaza ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mousa Faki Mahamat alisema mashambulizi hayo hayakubaliki na yana kiuka haki za binadamu na kutaka vita hivyo dhidi ya Wapalestina kusitishwa mara moja.
Mahamat aliongeza kuwa, watu wa Palestina wana “uungaji mkono kamili na usioyumba’’ wa AU.
“Afrika inalaani vita vya Gaza na inataka visitishwe mara moja kwasababu, siyo vya haki na vinakiuka haki za binadamu. Kama NAM, sote tunapaswa kusimama kidete na kulazimisha haki ya kimataifa na sheria za kimataifa kwa watu wote wanaopigania uhuru.”
Mahamat alisema hayo muda mfupi baada ya Uganda chini ya uongozi wa Rais Yoweri Museveni kuchukua rasmi wadhifa wa uenyekiti wa zamu wa miaka mitatu wa Vuguvugu hilo, kundi kubwa zaidi la mataifa duniani baada ya Umoja wa Mataifa.
Israel ilianzisha mashambulizi yake huko Gaza kujibu shambulizi la Hamas Oktoba 7, 2023 ambalo liliripotiwa kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1200. Tangu wakati huo, zaidi ya watu 24,000 wengi wao wanwake na watoto, wameuawa huko Gaza kulingana na wizara ya afya inayomilikiwa na Hamas
Hamas iliorodheshwa kama kundi la kigaidi na Israel na mataifa mengi ya Magharibi ikiwemo Marekani.
Mkutano huo ambao ulianza tarehe 15 Januari 2024 jijini Kampala ulianza na hotuba za wawakilishi wa mataifa wanachama ambapo Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini Grace Naledi Mandisa Pandor aliyaomba mataifa wanachama kuunga mkono kesi iliyowasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya Israel, kwa madai ya kutekeleza mauaji ya kimbari ampapo mataifa hayo yaliunga mkono hoja hiyo.
Mkutano huo wa kilele wa siku tano ulianza Jumatatu chini ya kauli mbiu: ‘’Kukuza Ushirikiano kwa Ustawi wa Pamoja wa Kimataifa’’.
Imetayarishwa na Sadam Muballe, VOA Kampala, Uganda.