Vikosi maalumu vya jeshi la Tunisia vimepambana vikali Jumapili na wanamgambo wanaomtii rais aliyeondolewa madarakani, Zine el-Abidine Ben Ali, huku waziri mkuu nchini humo akiahidi kutangaza serikali mpya ya umoja wa kitaifa Jumatatu.
Mapigano yalizuka Jumapili mchana karibu na makazi ya rais kiasi cha kilomita 15 kaskazini ya mji mkuu Tunis. Vyanzo vya jeshi huko Tunisia vinasema jeshi na walinzi wepya wa rais walijibu na kurudisha nyuma mashambulizi kutoka kwa wanamgambo wanaomtii Bw. Ben Ali. Mapigano mengine yalizuka mbele ya makao makuu ya chama kikuu cha upinzani na kwengineko huko Tunis, siku mbili baada ya kiongozi wa utawala wa kimabavu kukimbia uhamishoni.
Kufikia Jumapili mji mkuu wa Tunisia ulikuwa shwari karibu sawa na siku iliyotangulia, kukiwa na milio ya risasi na helikopta zikizunguka mji. Vyombo vya habari vimeripoti mapigano baina ya majeshi ya usalama na waasi wenye silaha karibu na makazi ya rais yaliyopo kwenye mtaa wa Carthage huko mjini Tunis, na pia katika sehemu kadhaa katikati ya mji mkuu.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa baadhi ya asakari wa ulinzi wa rais walihusika katika mapigano ya Carthage. Majeshi ya usalama yameripotiwa kuwatia nguvuni dazeni za watu.
Hapo Jumapili, mwandishi wa kifaransa alifariki dunia kufuatia majeraha aliyoyapata baada ya kupigwa na bomu la kutoa machozi wakati wa vurugu za Ijumaa. Shirika la Waandishi habari Wasio na Mipaka, RSF, limeripoti kuwa polisi walimlenga kwa makusudi.
Mapema Jumapili, mji ulionekana kurejea katika hali ya kawaida. Hakukuwa na magari mengi mitaani na kulikuwa na maduka na migahawa michache iliyokuwa imefunguliwa. Wakazi wa Tunis walichana mabango ya rais wa zamani Zine el-Abidine Ben Ali, ambaye aliikimbia nchi siku ya Ijumaa baada ya upinzani mkubwa.
Wakati huo huo, wale waliobaki madarakani, hasa kaimu Rais Fouad Mebazaa, walifanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano hadi pale nchi itakapofanya uchaguzi ambao umependekezwa kufanyika katika kipindi cha miezi miwili ijayo. Serikali mpya inatarajiwa kutangazwa Jumatatu.
Majadiliano ya kisiasa yalikuwa yakiendelea katika mgahawa katikati ya mji wa Tunis, ambapo wanaume walikuwa wakitathmini juu ya nani atakuwa rais ajaye.