Mvua kubwa imenyesha nchini humo, hususani maeneo yenye ukame yaliyoko kaskazini, katika siku za hivi karibuni, na kusababisha maji ya mafuriko kuingia majumbani, huku matukio kama hayo yakionekana katika maeneo mengine ya Afrika Mashariki.
Picha zilizoonyeshwa kwenye vyombo vya habari vya ndani zimeonyesha maji ya mafuriko yamefunika vijiji vyote na kuwafanya wakaazi kukimbilia kwenye maeneo ya mwinuko.
Hali mbaya ya hewa imewaathiri takriban watu milioni mbili na kusomba maelfu ya mifugo nchini Kenya, Somalia, Tanzania Uganda Burundi, Ethiopia, Djibouti na Sudan Kusini.
"Kufikia jana, nyumba 15,264 zimeathiriwa, wakati watu 15 wakiripotiwa kufariki," Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilisema kupitia mtandao wa X, uliokuwa ukijulikana kama Twitter.
Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katika maeneo ya Somalia yamewakosesha makazi watu 113,000 na "kuwaathiri" kwa muda” maelfu, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (UNOCHA) ilisema Jumatatu.
Tangu msimu huu wa mvua kuanza, zaidi ya watu 20 wamekufa na wengine zaidi ya 12,000 wamelazimika kuondoka kwenye makazi yao katika mkoa wa Somalia nchini Ethiopia kutokana na mafuriko, serikali ya mkoa ilisema mwishoni mwa wiki.