Mashambulizi hayo yalitokea Jumanne. Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kusini imesema kuwa wanne kati ya waliouawa walikuwa wenye asili ya Korea.
Shambulizi la kwanza lilitokea katika jengo la biashara lililo katika mji wa Acworth, takriban kilomita 50 kaskazini mwa mji mkuu wa jimbo hilo, Atlanta, ambapo, kwa mujibu wa mamlaka, watu wanne waliuawa.
Saa moja baadaye polisi mjini Atlanta waliwapata wanawake watatu wa asili ya Korea wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi ndani ya jengo lilokuwa na biashara ya saluni, na mwili wa mwanamke mwingine kupatikana karibu na eneo hilo.
Polisi wamesema walifukuzana na mshukiwa, Robert Aaron Long, mwenye umri wa miaka 21, ambaye alikuwa akiendesha gari lake, na hatimaye kumtia mbaroni, takriban kilomita 240, kusini mwa mjia wa Atlanta.
Mashambulizi hayo yanajiri wakati ambapo hali ya taharuki imeendelea kupanda katika sehemu mbalimbali hapa Mrekani, kufuatia ongezeko la mashambulizi yanayolenga watu wa asili ya Asia.
Matukio hayo yamekuwa yakilaaniwa vikali na baadhi ya wanasiasa, na viongoizi wa jamii zilizo na wakazi wengi kutoka bara Asia.