Msafara wa Taasisi ya Hifadhi ya Mazingira DRC washambuliwa

Watu wakitembea kwenye barabara kuu katika kijiji cha Muheto huko Kivu Kaskazini, Machi 28, 2022. Picha na ALEXIS HUGUET / AFP.

Washambuliaji waliwauwa takriban walinzi watatu huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo siku ya Alhamisi, afisa alisema.

Tukio hilo lilitokea karibu na hifadhi ya taifa ambayo ni makazi ya nusu ya idadi ya sokwe wa mlimani waliopo ulimwenguni ambao wako hatarini kutoweka, eneo hilo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara na wanamgambo.

Mhandisi mmoja aliripotiwa kutoweka na watu watatu kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, ambayo yalifanyika wakati magari ya Taasisi ya Hifadhi ya Mazingira Congo (ICCN) yalipokuwa yakiondoka kwenye kijiji cha Kivandya katika Jimbo la Kivu Kaskazini, ambako dazeni makundi ya wanamgambo wenye silaha wanafanya harakati zao.

"Hatujui wahusika ni akina nani," alisema msimamizi wa eneo hilo Alain Kiwewa, na kuongeza kuwa washambuliaji walichukua silaha wakati wakikimbia.

ICCN haikujibu mara moja ombi la maoni hayo.

Virunga imejikuta katikati ya harakati za wanamgambo ikiwa ni mabaki kutoka vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyopiganwa takriban mwanzoni mwa karne.

Taasisi hiyo ilionya kuhusu kuzuka upya kwa ghasia mwezi Februari baada ya washukiwa wanamgambo wa Mai Mai waliposhambulia maskani ya walinzi huko Virunga, ambapo mtu mmoja aliuwawa na wawili kujeruhiwa.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la Reuters.