Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amenukuliwa na gazeti la Mwananchi akisema wanaoshikiliwa na jeshi hilo kufuatia kutekwa nyara mfanyabiashara huyo ni 12 hadi sasa.
Wakati huohuo msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara, amesema familia na bodi ya kampuni ya Dewji imekutana Alhamisi na kumuombea, lakini pia inaliachia Jeshi la Polisi jukumu la kutoa taarifa zote zinazo husika na tukio hilo.
Gazeti la Nipashe pia limeripoti kuwa familia imeshtushwa na kusikitishwa na taarifa za uzushi zilizo tolewa na mitandao ya kijamii kuwa Mo amepatikana.
“Familia na Bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Simba na wanachama kwa ujumla tuendelee na dua za kuhakikisha ndugu yetu anapatikana akiwa mzima na wale wote waliohusika wanakamatwa ili kuchukuliwa hatua," amesema.
Pia amesema jana walikuwa na Mo kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kujadili maendeleo ya klabu hiyo na mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa ni saa 5:00 usiku.