Baada ya kuachiwa kutoka polisi Oysterbay Jumamosi, Roma Mkatoliki amesema kutokana na makubaliano yao na polisi katika kuachiwa kwao wameomba kuvuta muda kidogo hadi kesho ambapo watatoa taarifa zaidi.
Roma akiongea baada ya kutoka hospitali ya Mwananyamala amewaomba wafuasi wao na wapenzi wa muziki na Watanzania kuwapa fursa ya kupumzika leo na kesho na Jumatatu wataongea kwa kina yote yaliowapata.
Ametoa shukrani zake za dhati kwa msaada wote walioupata katika shinikizo la kuwatafuta, na kusema kwamba yeye na wenziwe wako katika hali nzuri.
Hata hivyo msanii huyo na wenzie walionekana ni wenye uchovu na mshituko mkubwa baada ya kuachiwa wakati wakiongea na waandishi wa habari.
Msanii Roma Mkatoliki alifikishwa na wenzie Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam Jumamosi kwa mahojiano.
Lakini hata hivyo bado hakuna maelezo ya kutosha kuhusiana na wapi alipokuwa na wenzake na nani aliyekuwa anawashikilia.
Kupatikana kwao kumefuatia wito mkubwa uliokuwa umetolewa na wasanii na mashabiki nchini kuhusu kuachiliwa kwake huru, ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Simon Sirro wiki illiopita alitoa tamko kwamba bado walikuwa wakiendelea na upelelezi wa tukio la kupotea kwa msanii huyo na wenzake.