Vyanzo vya habari nchini Tanzania vinasema kuwa kupatikana kwa Roma kumethibitishwa pia na Mkurugenzi wa Tongwe Records J. Mada.
Lakini hata hivyo bado hakuna maelezo ya kutosha kuhusiana na wapi alipokuwa na wenzake na nani aliyekuwa anawashikilia.
Kwa sasa habari zilizotufikia ni kuwa yupo kituo cha polisi kwa taratibu za kipolisi kwa kuwa jalada la kupotea kwao lilifunguliwa hapo.
Kupatikana kwao kumefuatia wito mkubwa uliokuwa umetolewa na wasanii na mashabiki nchini kuhusu kuachiliwa kwake huru, ndani na nje ya mitandao ya kijamii.
Kabla ya hapo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Simon Sirro alitoa tamko kwamba bado walikuwa wakiendelea na upelelezi wa tukio la kupotea kwa msanii huyo na wenzake.