Hali mbaya ya hewa ilivuruga mipango ya safari ya Charles na Malkia Camilla na kuwafanya wapande bajaji ya umeme maarufu kama ‘Tuktuk’ kwenda Fort Jesus, eneo la Turathi ya Dunia la UNESCO la miaka 400 katika Mji Mkongwe wa Mombasa.
Badala yake, wanandoa hao wa kifalme walisimama kwa muda mfupi na kupiga picha ndani ya gari la magurudumu matatu, ambalo lilikuwa limepambwa kwa muundo wa Kiafrika na nembo ya Union Jack.
Pwani ya Kenya na maeneo mengine ya nchi yamekuwa yakikumbwa na mvua kubwa na wakati mwingine katika siku za hivi karibuni kumekuwa na mafuriko.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya kibinadamu, OCHA, lilisema mwezi uliopita kuwa Afrika Mashariki imekuwa ikikumbwa na mvua kubwa kuliko kawaida katika kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Desemba kwa sababu ya hali ya El Nino.
El Nino ni mwenendo wa kiasili unaotokea unahusishwa na ongezeko la joto duniani kote, pamoja na ukame katika baadhi ya sehemu duniani na mvua kubwa katika maeneo mengine.
Mfalme Charles kwa muda mrefu amekuwa mwanamazingira mwenye bidii na programu yake katika ziara hiyo ya siku nne nchini Kenya imeangazia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, pamoja na kuunga mkono sanaa ya ubunifu, teknolojia na vijana.
"Ikiachwa bila kudhibitiwa, ongezeko la joto duniani, upotevu wa viumbe hai na mabadiliko ya hali ya hewa ni changamoto ambazo ni tishio kwetu sote na zinaweza tu kukabiliwa na jamii nzima inayofanya kazi pamoja kwa moyo wa vitendo, ushirikiano na kwa kujitolea," alisema akiwa katika ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini huko Nairobi wiki hii.
Ziara hiyo nchini Kenya hata hivyo imeibua hisia mseto katika koloni hilo la zamani, huku wito ukimtaka mfalme huyo kuomba radhi kutokana na ukandamizaji wa kikatili wa Uingereza katika harakati za kupigania uhuru wa taifa hilo.
Katika hafla ya serikali siku ya Jumanne, mfalme huyo mwenye umri wa miaka 74 alisema "makosa ya siku za nyuma yanasababisha huzuni kubwa na majuto makubwa," lakini hakuomba msamaha.
Takriban watu 10,000 -- hususani kutoka kabila la Kikuyu -- waliuawa wakati wa enzi za utawala wa kikoloni zilipoukandamiza kikatili uasi wa Mau Mau kati ya mwaka 1952 hadi 1960, ingawa baadhi ya watu wameziongeza takwimu hizo za kweli kuwa juu zaidi.
Maelfu zaidi walikusanywa na kuzuiliwa bila kufunguliwa mashtaka katika kambi ambapo ripoti za kunyongwa, kuteswa na kupigwa vibaya zilikuwa za kawaida.
Wakati alipokuwa Nairobi, mfalme alifanya mazungumzo ya faragha na vizazi vya Dedan Kimathi na Mekatilili wa Menza -- viongozi wawili mashuhuri katika kupigania uhuru.
Siku ya Ijumaa, Charles alitembelea Msikiti wa Mandhry mjini Mombasa na Kanisa Kuu la Ukumbusho, ambako alijumuika katika mkutano uliojumisha madhehebu mbalimbali.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP