Mfalme Charles III wa Uingereza awasili Kenya

Mfalme Charles wa Uingereza na mkewe Malkia Camilla.

Mfalme Charles wa tatu na mkewe Malkia Camilla waliwasili nchini Kenya Jumatatu usiku kwa ziara ya siku nne.

Wawili hao walipokelewa katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi na mkuu wa Baraza la Mawaziri, ambaye pia ni waziri wa Mambo ya Nje, Musalia Mudavadi na balozi wa Uingereza nchini Kenya, Neil Wigan.

Ni ziara ya kwanza ya Mfalme Charles nchini Kenya tangu alipochukua usukani baada ya mama yake, Malkia Elizabeth II, kufariki Septemba 2022.

Hii pia ni ziara yake ya kwanza kama mfalme katika taifa la Jumuiya ya Madola, ambapo maoni yoyote atakayotoa juu ya historia ya ukoloni wa Uingereza yanatarajiwa kufuatiliwa kwa karibu, kwa mujibu wa wachambuzi.

Charles anatarajiwa kukabiliana na "masuala yenye maumivu makubwa" ya uhusiano wa kihistoria wa Uingereza na Kenya -- yaani kipindi cha utawala wa Uingereza, ambao ulimalizika mwaka 1963, Kasri ya Buckingham imesema.

Hii itajumuisha "Dharura" ya 1952-1960, wakati mamlaka ya kikoloni ilitangaza hali ya dharura ili kukabiliana na kampeni ya msituni ya Mau Mau dhidi ya walowezi kutoka Ulaya .

Mfalme wa Uingereza atalitembelea jiji la Nairobi pamoja na mji wa bandari wa Mombasa , lakini siyo mji wa Nanyuki ambako kuna kituo cha mafunzo ya jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK).