Mashambulizi ya anga yaendelea Khartoum

Moshi ukifuka katika jiji la Khartoum, tarehe 22 Mei 2023. Picha na AFP.

Jeshi la Sudan lilifanya mashambulizi ya anga katika mji mkuu Khartoum siku ya Jumatatu, wakaazi walisema, linataka kupata ushindi dhidi ya mahasimu wake wa kijeshi saa chache kabla ya sitisho la mapigano la wiki moja linalolenga kuruhusu usambazaji wa misaada kuanza kutekelezwa.

Jeshi pia liliendelea kufanya mashambulizi ya anga siku ya Jumapili jioni, mashuhuda walisema, mashambulizi hayo yalilenga magari kutoka vitengo vinavyohashimika vya vikosi vya Rapid Support Forces ambavyo vimekuwa vikifanya shughuli katika maeneo yanayokaliwa na watu katika mji mkuu huo tangu mzozo kati ya makundi hayo mawili ya kijeshi ulipozuka Aprili 15.

Pande zote mbili zimesema zitaheshimu makubaliano ya sitisho la mapigano kuanzia saa 9:45 alasiri. Ingawa mapigano yaliendelea licha ya makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano, hii ni mara ya kwanza usuluhishi kukubaliwa rasmi baada ya mashauriano.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yanajumuisha utaratibu wa kufuatilia unaohusisha jeshi na RSF pamoja na wawakilishi kutoka Saudi Arabia na Marekani, ambao walisimamia makubaliano hayo baada ya mazungumzo yaliyofanyika mjini Jeddah.

Makubaliano hayo yameongeza matumaini ya kusitisha vita hivyo ambavyo vimesababisha watu takriban milioni 1.1 kuhama makazi yao, wakiwemo watu zaidi ya 250,000 waliokimbilia nchi jirani, na kutishia kuyumbisha hali tete katiak kanda hiyo.

Mashambulizi ya anga katika makazi ya watu yameripotiwa siku ya Jumatatu huko Khartoum, Omdurman na Bahri, miji mitatu inayounda mji mkuu uliotenganishwa na makutano ya mto wa Blue Nile na White Nile. Pia mashuhuda hao walisema mapigano yaliweza kusikika katikati ya jiji la Khartoum.

Jeshi limejitahidi kuviondoa vikosi vya RSF kutoka maeneo muhimu yaliyoko katikati ya jiji la Khartoum na vitongoji venye majengo ya makazi ya raia.

Vikosi vya RSF, ambayo ni chimbuko la wanamgambo wanaohofiwa waliopigana na serikali huko Darfur, ni hodari katika mapigano ya ardhini, wakati jeshi linategemea kwa kiasi kikubwa mashambulizi ya anga na makombora.

Zaidi ya wiki tano za mapigano mjini Khartoum, mamilioni ya watu wamekwama katika nyumba au vitongoji vyao.

Wakazi wa Khartoum wameripoti ongezeko la vitendo vya uporaji na uvunjaji wa sheria pamoja uharibifu unaosababisha kukatika kwa umeme na maji. Usambazaji chakula umekuwa ukipungua katika baadhi ya maeneo, na hospitali nyingi zimefungwa.