Marekani na washirika wengine kuufuatilia kwa karibu uchaguzi mkuu Madagascar

Rais wa Marekani Joe Biden akiwa ikulu ya White House Septemba 17, 2023 Picha na Kent Nishimura / AFP.

Umoja wa Ulaya, Marekani na wanachama wengine wa jumuiya ya kimataifa walisema Jumanne kwamba wanafuatilia kwa "umakini mkubwa" maandalizi ya uchaguzi wa rais nchini Madagascar, kufuatia ya mizozo kuhusu taratibu za kanuni zake za uchaguzi.

Wawakilishi wa nchi nane na mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ufaransa na Japan, walisema "imani" katika mchakato wa uchaguzi ni muhimu ili matokeo ya uchaguzi utakaofanyika Novemba yakubalike β€œna wote, ” na kuhakikisha kuwepo kwa hali ya "utulivu" nchini.

"Walio saini mkataba, washirika wa kimataifa wa Madagascar, wanafuata kwa umakini mkubwa matukio ya hivi karibuni yanayohusiana na maandalizi ya uchaguzi wa rais," kundi hilo liliandika katika taarifa yake.

Taarifa hii imekuja baada ya upinzani kulalamikia "mapinduzi ya kitaasisi" kumpendelea rais wa nchi hiyo aliyekuwa madarakani Andry Rajoelina.

Wapiga kura nchini Madagascar, watapiga kura kumchagua rais tarehe 9 Novemba. Madagascar ni moja ya nchi maskini sana duniani licha ya kuwa na maliasili nyingi.

Rajoelina, 49, alijiuzulu mapema mwezi huu kwa mujibu wa katiba ili kugombea tena nafasi hiyo.

Rais wa Baraza la Seneti alipaswa kuchukua nafasi hiyo lakini alikataa kufanya hivyo kwa "sababu binafsi", na kuliachia jukumu hilo kwa "serikali ya pamoja" inayoongozwa na Waziri Mkuu Christian Ntsay, ambaye ni mshirika wa Rajoelina.

Hatua hiyo ilikubaliwa na mahakama kuu ya nchi hiyo, na kuibua hasira za upinzani.

Mahakama pia imetupilia mbali rufaa ya kutaka ugombea wa Rajoelina utangazwe kuwa batili kutokana na uraia wake wa nchi mbili za Ufaransa.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP