Mamlaka Nigeria yashutumiwa kutowatendea haki waandamanaji wa #EndSars

Mwandamanaji akiwa na bango kuadhimisha mwaka mmoja wa kulaani ukatili wa Polisi dhidi ya waandamanaji wa EndSars, Abuja, Nigeria ,Oct. 20, 2021.

Mamlaka ya Nigeria imeshutumiwa kwa kushindwa kuhakikisha haki inatendeka kwa mauaji ya waandamanaji wa #EndSars mwaka 2020 miezi sita baada ya jopo la mahakama kuvihusisha vikosi vya usalama.

Human rights watch iliitaka serikali kuchukua hatua kutokana na mapendekezo yake na kuwawajibisha wahusika wa makosa hayo.

Katika taarifa yake, Human Rights imesema serikali kushindwa kuchukua hatua kwa mapendekezo ya jopo kutatoa ujumbe wenye uchungu kwa waathirika na kuhatarisha ghasia zaidi kufanywa na maafisa wa usalama.

Mamia ya vijana waliingia katika miji mikuu nchini Nigeria mwezi Octoba mwaka 2020 kutaka kitengo cha polisi kuvunjwa kinachojulikana kama kitengo maalumu cha kupambana na ujambazi, kwenye vuguvugu lililohamasisha #EndSars.

Maafisa wa usalama walishutumiwa kujibu kwa kutumia nguvu kupita kiasi ikiwemo kufyatua risasi.

Moja ya ukandamizaji mkubwa ni ule uliotokea katika Lekki toll gate, mjini Lagos wakati maafisa wa jeshi na polisi waliporipotiwa kuwafyatulia risasi na kusababisha mauaji katika kundi la waandamanaji.

Jopo lililoundwa na serikali ya Lagos kufuatia maandamano ya mwezi Novemba mwaka jana liligundua kwamba vikosi vya usalama viliwapiga risasi, kuwajeruhi na kuwauwa waaandamanaji ambao hawakuwa na silaha.