Afrika Kusini yaridhika na uwamuzi wa ICJ kuiamrisha Israel kuzuia uwezekano wa mauaji ya kimbari Gaza

Mahakama ya Sheria ya Kimataifa inatoa uwamuzi kuhusu hatua za dharura kwa gaza katika kesi ya mauwaji ya kimbari dhidi ya Israel, mjini The Hague

Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa amesema kwamba tuhuma za uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza “umewekwa wazi” na uwamuzi wa Mahakama ya Sheria ya Kimataifa siku ya Ijumaa.

Ramaphosa ameongezea kusema kwamba nchi yake, iliyowasilisha kesi ya mauwaji ya kimbari dhidi ya Israel, mbele ya mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa, imefurahi kwamba "kilio cha wananchi wa Palestina kutendewa haki kimesikika na chombo cha kuheshimiwa cha Umoja wa mataifa."

Rais Cyril Ramaphosa akiwa na furaha baada ya uwamuzi wa ICJ.

Majaji wa mahakama ya ICJ, katika uwamuzi wa awali wameimarisha Israel kufanya kila iwezalo kuzuia vifo, uharibifu na hatua zozote za mauwaji ya kimbari katika mashambulizi yake ya Gaza, lakini hawakuiamrisha Israel kusitisha mapigano, jambo Afrika ya Kusini ilihimiza kutangazwa.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amekosoa vikali uwamuzi huo akisema haukubaliki. Anasema daima Israel inadhamira ya dhati kuheshimu sheria za kimataifa na hatua hii ni jaribio la kuizuia nchi hiyo kutumia haki yake ya kujilinda.

Maafisa wa Palestina wamepongeza uwamuzi huo wakisema ni ushindi mkubwa kwa wakazi wa Gaza.

Viongozi wa Hamas wanasema wataheshimu usitishaji vita ikiwa Israel itafanya hivyo, licha ya kwamba mahakama hiyo ya kimataifa haikutaja suala la usitishaji mapigano.

watu walokusanyika nje ya mahakama ya ICJ wakishukuru uwamuzi wa majaji kuhusiana na kesi dhidi ya Israel iliyofikishwa na Afrika Kusini,. Januari 26, 2024.

Sehemu kubwa ya Jumuia ya Kimataifa na wanaharakati na watu wanaopigania kusitishwa kwa mapigano wamepongeza uwamuzi wa IJC.

Mahakama hiyo imeitaka pia Israel kuharakisha kupelekwa kwa msaada wa dharura kwa wananchi wa Gaza na kuchukua hatua nyenginezo za haraka kuzuia madhila yanayowakumba wananchi wa Gaza.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.