Valeriy Tkachov, Naibu mkurugenzi wa idara ya biashara katika Shirika la Reli la Ukraine, alisema kupitia ukurasa wa Facebook kwamba katika wiki iliyopita idadi ya mabehewa ya nafaka yaliyoelekea bandari za Odesa yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 26 kutoka 4,227 hadi kufikia 5,341.
Alisema hadi mabehewa 970 yamekuwa yakishusha nafaka kwenye ghala katika bandari hizo kila siku.
Wiki moja kabla idadi ya magari iliongezeka kwa karibu asilimia 50. Mwezi Agosti, Ukraine ilizindua "nji ya kibinadamu" kwa meli zinazoelekea katika masoko ya Afrika na Asia ili kujaribu kukwepa kizuizi kilichopo katika bahari ya Black sea, baada ya Russia kujitoa katika makubaliano ambayo yalikuwa yakiihakikishia Kyiv usafirishaji nje wa nafaka kwa njia ya bahari wakati wa vita.
Baadaye, afisa mwandamizi wa kilimo alisema njia hiyo - ambayo inapita katika pwani ya Kusini Magharibi mwa bahari ya Black sea iliyoko Ukraine, kuingia katika eneo la bahari la Romania na kwenda hadi Uturuki - pia itatumika kwa usafirishaji wa nafaka.
Naibu Waziri Mkuu Oleksandr Kubrakov alisema Alhamisi meli 91 zilisafirisha tani milioni 3.3 za bidhaa za kilimo na chuma tangu ukanda huo uanze kufanya kazi mwezi Agosti.