Maandamano ya Iran: Maafisa wa usalama wakiri Idadi ya vifo ni 17

Sept. 21, 2022, Picha hii imepigwa na mtu binafsi siyo mfanyakazi wa shirika la habari la AP wala shirika la habari la AP: Waandamanaji wakiwasha moto na kuzuia barabara wakati wa maandamano nchini Iran.

Serikali ya Iran inajibu vikali kwa kutumia nguvu kupita kiasi, na kuwakamata waandamanaji kote nchini baada ya kufariki kwa msichana akiwa amezuiliwa katika kituo cha polisi.

Polisi wanadai kuwa msichana huyo Mahsa Amini alikuwa hajavaa hijabu inavyotakikana, huku maafisa wa usalama wakikiri kuwa takriban watu kumi na saba wameuawa katika siku kadhaa za vurugu.

Katika kauli mbalimbali zilizochapishwa Jumatano, maafisa wa Iran walisema watu wanne waliuawa katika matukio kadhaa ya ghasia katika jimbo la kaskazini magharibi la Kurdistan huku wengine wawili waliuawa wakifanya ghasia katika jimbo jirani la Kermanshah.

Maafisa wa usalama wa Iran wamewalaumu vibaraka wanaopinga mapinduzi ya Kiislamu kwa ghasia hizo. Lakini shirika la haki za binadamu lenye makao yake London, Amnesty International, limesema Jumatano lilikuwa na ushahidi kuwa vyombo vya usalama vya Iran vimewasambaza waandamanaji wengi wao walikuwa watulivu kwa kutumia njia kinyume cha sheria, kama vile kutumia risasi za kuua ndege na vipande vingine vya chuma, mabomu ya machozi na maji ya mwasho, na kuwapiga watu kwa virungu.

Maandamano yafanyika katika mji mkuu Tehran baada ya msichana Mahsa Amini kufariki akiwa ameshikiliwa katika kituo cha polisi nchini Iran.

Repoti ya Amnesty International ilisema kikundi hicho kimesajili mauaji ya waandamanaji wanane yaliyofanywa na vyombo vya usalama Jumatatu na Jumanne, ikiwemo wanne huko Kurdistan, wawili huko Kermanshah na wawili wengine Magharibi mwa jimbo la Azerbaijan. Imesema waliokufa ni wanaume sita, mwanamke mmoja na mtoto mmoja.

Shirika hilo haki za binadamu kimesema mamia zaidi ya watu, wakiwemo watoto, wamekamatwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi na wamepata majeraha yenye maumivu makali kutokana na risasi za ndege na silaha nyingine.

“Katika baadhi ya maeneo, baadhi ya waandamanaji walihusika na kutupa mawe nakuharibu magari ya polisi. Hili halihalalishi utumiaji wa risasi za chuma, ambazo zimepigwa marufuku katika hali yoyote kutumika,” Amnesty International iliongeza.

Jimbo la Kurdistan lilikuwa ni nyumbani kwa mwanamke wa Kikurdi mwenye asili ya Iran umri miaka 22, Mahsa Amini aliyefariki Tehran tarehe 16, mwezi Septemba, siku tatu baada ya polisi wanaosimamia maadili kumkamata kwa madai ya kuonyesha sehemu kubwa ya nywele zake hadharani wakati akitembelea mji mkuu wa Iran.

Amini alikuwa katika hali mahtuti mara baada kukamatwa akiwa na wanawake wengine katika kituo kimoja cha polisi mjini Tehran na baadae alifariki hospitalini, kulingana na taarifa kutoka kwa familia yake na hospitali. Familia yake imeshutumu mamlaka husika kwa kumshambulia mtoto wao, lakini polisi wamekanusha kumtendea uovu wowote na kusema bila ya kuonyesha ushahidi kuwa alipata mshituko wa moyo. Ndugu zake walisema Amini alikuwa hana historia ya matatizo hatarishi ya kiafya.