Waziri wa mambo ya nje wa Iran mapema wiki hii amesema kwamba mazunguzo yanaendelea na Saudi Arabia kuelekea kurejesha uhusiano wa kidiplomasia pia. Uhusiano kati ya Iran na UAE pamoja na Saudi Arabia ulivujika 2016 kufuatia kuuwawa kwa kiongozi wa kidini kwa kishia kutoka Saudi Arabia Nimr al Nimr.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani amewaambia wanahabari mwanzoni mwa wiki kwamba hali inaendelea kuboreka kieneo, matumaini yakiongezeka ya kurejeshwa tena kwa uhusiano na Saudi Arabia. Iraq na Oman wote wamekuwa mstari wa mbele japo siyo kwa njia rasmi katika kuongoza mazungumzo kati ya Tehran na Riyadh.
Paul Sullivan ambaye ni mchambuzi wa masuala ya mashariki ya kati kutoka baraza la Atlantic ameiambia VOA kwamba biashara kati ya Iran na UEA ilikuwa bora zaidi 2017, lakini ikashuka mara moja baada ya uhusiano kuvunjwa. Asemema kwamba kuna kati ya watu laki 5 hadi 6 kutoka Iran wanaoishi Dubai. Ameongeza kusema kwamba hata hivyo vikwazo vya Marekani vingali vinafanya kazi kwa raia wa Iran walioko UAE licha ya hatua zilizopigwa za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia.