Lugola awahakikishia mabalozi Tanzania ni salama

Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Kangi Lugola, amekutana na mabalozi wa Italia, Kenya na Afrika Kusini jijini Dar es Salaam, Alhamisi na kuwahakikishia kuwa hali ya ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao uko vizuri.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe Lugola aliwahakikishia mabalozi hao kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama kwa kuwa wizara yake imejipanga kuendelea kuwalinda raia na mali zao pamoja na wageni wote waishio nchini.

“Mheshimiwa Balozi, nashukuru sana kwa kunitembelea. Najisikia furaha kwa ujio wako na karibu sana wakati wowote. Wizara yangu pamoja na nchi kwa ujumla tutaendelea kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali,” amesema Lugola wakati wa mazungumzo hayo na Balozi wa Afrika Kusini nchini, Thami Mseleku.

Kwa upande wake, Balozi Mseleku alisema akiwa nchini anajiona kuwa yuko nyumbani kwa sababu nchi yake ina historia kubwa ya ushirikiano na Tanzania.

Balozi wa Italia, Roberto Mengoni, alimpongeza Waziri Lugola kwa kuteuliwa na Rais John Magufuli kuiongoza wizara hiyo na pia alimhakikishia ushirikiano zaidi kati ya nchi yake na Tanzania.

Kwa upande wake Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu, alisema Tanzania ni nchi yake na anajisikia furaha kuwapo nchini kwa sababu alishawahi kufanya kazi miaka kadhaa iliyopita nchini, hivyo nchi yake itaendelea kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali Tanzania.