Walid Alorafi, msemaji wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID) mjini Benghazi, alisema kulingana na baadhi ya wahamiaji, walizuiliwa mateka hadi miezi saba na "walitaka kwenda Ulaya."
Wahamiaji hao wanatoka mataifa mbalimbali kusini mwa jangwa la Sahara lakini hasa kutoka Somalia, Alorafi alisema.
"Tulivamia maficho katikati mwa jiji la Kufra jana usiku na tukapata wahamiaji haramu wakiwemo wanawake, watoto na wazee ambao wengine wana alama za mateso na risasi," Alorafi alisema.
"Wahamiaji hao wote wamekabidhiwa kwa mawakala wa uhamiaji haramu kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya taratibu," Alorafi aliongeza.
CID ilichapisha picha za video za kikosi chao kikibomoa nyumba walimozuiliwa wahamiaji hao. Kanda zingine ni pamoja na picha za wahamiaji wakiwa na alama za mateso kwenye miili yao. Baadhi ya wahamiaji walionekana wakibebwa kuelekea kwenye gari la wagonjwa na wafanyakazi wa misaada.
Kufra iko takriban kilomita 1,712 kutoka mji mkuu Tripoli.
Libya imekuwa njia ya kupitia kwa wahamiaji wanaokimbia migogoro na umaskini kuelekea Ulaya kupitia njia hatari ya kuvuka jangwa, na hatimaye bahari ya Mediteranian kufuatia kupinduliwa kwa Muammar Gaddafi katika uasi ulioungwa mkono na NATO mwaka 2011.
Uchumi wake unaotegemea mafuta pia ni kivutio kwa wahamiaji wanaotafuta kazi.
Libya yenye utajiri wa mafuta ni makazi ya wahamiaji 704,369 kutoka zaidi ya mataifa 43, kulingana na data iliyokusanywa katika manispaa 100 za Libya katikati ya 2023, takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha.
Mwezi Machi, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji lilisema takriban miili 65 ya wahamiaji iligunduliwa katika kaburi la pamoja kusini magharibi mwa Libya na CID.
"Ninaomba ushirikiano wa kikanda uimarishwe ili kuhakikisha ulinzi wa wahamiaji," alisema mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Abdullah Bathily katika mkutano wake na Baraza la Usalama mwezi Aprili.