Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 05:20

Makazi ya Waziri Mkuu wa Libya yashambuliwa


Maadamano nchini Libya
Maadamano nchini Libya

Makazi ya waziri mkuu wa Libya Abdulhamid al-Dbeibah yalishambuliwa kwa maguruneti ya kurushwa kwa roketi Jumapili katika shambulio ambalo halikusababisha majeruhi, waziri mmoja wa Libya ameliambia shirika la habari la Reuters.

Waziri huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alithibitisha katika ujumbe kwamba shambulio hilo lilisababisha uharibifu mdogo. Waziri huyo hakutoa maelezo zaidi.

Raia wawili wamesema walisikia milipuko mikubwa karibu na bahari katika kitongoji cha kifahari cha Hay Andalus cha mjini Tripoli, ambako ni makazi ya waziri mkuu Dbeibah.

Raia mwingine amesema baada ya milipuko hiyo mikubwa kusikika, maafisa wengi wa usalama na magari yao walipelekwa karibu na eneo hilo.

Libya haijapata amani au utulivu tangu uasi wa 2011 ulioungwa mkono na NATO, na iligawanyika mwaka wa 2014 kati ya pande za mashariki na magharibi, na tawala hasimu zikiongoza kila upande.

Serikali ya umoja wa taifa ya Dbeibah iliundwa kupitia mchakato ulioungwa mkono na Umoja wa mataifa mwaka 2021 lakini bunge huko mashariki, lilipinga kutambua uhalali wa serikali hiyo mwishoni mwa mwaka baada ya jaribio ambalo halikufanikiwa la kuanda uchaguzi wa taifa, hali ambayo ilisababisha mzozo wa kisiasa wa muda mrefu.

Mapema mwezi Machi, viongozi watatu wakuu walisema walikubaliana juu ya “umuhimu” wa kuunda serikali mpya ya umoja ambayo itasimamia uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu.

Dbeibah aliapa kuwa hatokabidhi madaraka kwa serikali mpya bila uchaguzi wa taifa kufanyika.

Forum

XS
SM
MD
LG