Lagos na majimbo mengine yaendelea kuwa chini ya amri ya kutotoka nje

Alister, muandamanaji anasemaa yake Emeka aliuawa na risasi iliyokuwa haikumkusudia iliyorushwa na jeshi, alipokuwa akieleza hisia zake kwa shirika la Associated Press, Lagos, Nigeria, Jumanne Oct. 20, 2020.

Jiji kubwa la Nigeria, Lagos na majimbo kadhaa yanaendelea kuwa chini ya amri ya kutotoka nje Alhamisi kutokana na maandamano dhidi ya ukatili unaofanywa na polisi kufuatia ghasia Jumatano.

Milio ya bunduki ya hapa na pale imekuwa ikisikika Jumatano usiku licha ya wito wa rais kutaka maelewano na utulivu kudumishwa nchini humo.

Kutokana na maandamano na ghasia hizo viongozi mbali mbali wa dunia wameitaka serikali ya Nigeria kuzuia ghasia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani mashambulizi ya polisi dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani.

Katibu Mkuu huyo amelaani ukatili unaofanywa na polisi wakati shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International likitoa ripoti kwamba watu 12 waliuliwa pale polisi walipowashambulia waandamanaji katika maeneo mawili tofauti siku ya Jumanne.

Akizungumza na shirika la habari la AP, Guterres amesema kunahaja ya kusitisha ukatili unaofanywa na polisi.

Katibu Mkuu anaeleza : "Kwa hivyo wakati umefika kwa mataifa yote kufahamu na nina matumaini Nigeria pia itafahamu kwamba ukatili unaofanywa na polisi inabidi kusitishwa, na wale watakaohusishwa na vitendo hivyo viovu inabidi kuwajibishwa na ni muhimu kufanyika kila mahali duniani."

Guterres alikuwa akizungumza wakati shirika la Amnesty International linatoa ripoti kuhusu ghasia zilizozuka kwenye kituo cha kulipisha ada kwenye barabara kuu ya Lagos Jumanne usiku na kulaaniwa kimataifa.

Mkurugenzi mkazi wa Amnesty International, Osai Ojigho akitoa ripoti hiyo ametoa wito kwa wakuu wa serikali kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Mkurugenzi Mkazi wa Amnesty International nchini Nigeria anaeleza : "Kwa hakika wito wetu kwa wakuu ni kuwataka kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na suala hili kufahamu nini kilichotokea, nini kilichosababisha wanajeshi kuwepo hapo na kuwashambulia waandamanaji. Lakini zaidi ya hapo tunasisitiza kwamba chini ya sheria ya kimataifa ikiwa unataka kuwaondosha watu wanaolalamika kwa amani kuna njia na utaratibu wa kufuata na sio kuwafyatulia risasi."

Ripoti ya Amnesty International inaeleza kwamba watu 56 wameuliwa mnamo wiki mbili za maandamano yaliyoenea kote nchini kupinga utumiaji nguvu wa polisi. ikiwa ni pamoja na hao 12 waliouliwa siku ya Jumanne.

Maandamano yaliyoanza kudai kuvunjwa kwa kikosi maalum cha polisi cha SARS yamendelea licha ya amri ya kutotoka nje kutangazwa katika majinbo zaidi ya sita na kuzuka kwa ghasia.

Hivi sasa waandamanaji wanadai mageuzi ya kiuchumi na kupambana na umaskini na ukosefu wa ajira. Sunday Michael mfanyabiashara wa Lagos anasema kwa bahati mbaya serikali haitetei maslahi ya wananchi.

Sunday Michael anaeleza : "Maslahi ya binafsi mbele ya maslahi ya kitaifa, unanipata? Hili ndilo tatizo la Nigeria. Na kile tulichoshuhudia Jumanne, ni kwa sababu ya maslahi binafsi ya mwanasiasa, kwani biashara yake ilikuwa hatarini kwa kukosa mapato kutokana na ulipaji ada kwenye kituo hicho."

Kituo hicho kwenye barabara kuu ya Lagos ndio kimekuwa kitovu cha mkusanyiko mkubwa wa waandamanaji wanaodai mageuzi kamili ya kiuchumi na kisiasa huko Nigeria hasa kutokana na kudorora kwa uchumi kutokana na janga la corona.

Milio ya bunduki imendelea kusikika Alhamisi mjini Lagos na moshi mkubwa ulionekana ukitanda kutoka jela kuu ya lagos. Biashara na maduka katika jiji hilo yamendelea kufungwa.

Mshauri wa Rais Muhamadu Buhari anasema kwamba rais amekuwa akikutana hii leo na wakuu wa usalama wa kitaifa kujadili namna ya kukabiliana na hali hiyo, katika taifa hilo kuu kiuchumi barani Afrika.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.