Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 16:05

Buhari awataka Wanigeria kuwa watulivu kufuatia ripoti za raia kupigwa risasi


Waandamanaji wajitokeza mjini Lagos, Nigeria, Tuesday Oct. 20, 2020, kupinga ukatili wa polisi.
Waandamanaji wajitokeza mjini Lagos, Nigeria, Tuesday Oct. 20, 2020, kupinga ukatili wa polisi.

Rais Muhammadou Buhari wa Nigeria ametoa wito wa kuwepo utulivu baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi waandamanaji katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos Jumanne usiku.

Wito wa rais umetolewa muda mfupi tu baada ya Gavana wa Jimbo la Lagos kukanusha kuuawa kwa waandamanaji waliokuwa wanakaidi amri ya kutotoka nje, lakini akikiri kwamba karibu waandamanaji 30 kati yao walijeruhiwa.

Wanigeria waliamka Jumatano wakiwa wameshtushwa na ripoti kwenye mitandao ya kijami inayoonyesha wanajeshi wakiwafyatulia risasi kwa karibu waandamanaji.

Habari kwenye mitandao ya kijamii za wanajeshi kuwarushia risasi kwa karibu waandamanaji elfu moja kwenye kituo cha kulipa ada kwenye barabara kuu katika mji mkuu wa kibiashara Lagos, kimewashtusha wa Nigeria na sehemu kubwa duniani. Kitendo ambacho Amnesty International na mashahidi wanadai kilifanywa na wanajeshi na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Akiwahutubia wakazi wa Lagos Jumatano mchana Gavana wa jimbo hilo Babajide Sanwo-Olu amesema watu 25 walijeruhiwa na wanapatiwa matibabu lakini hakuna aliyefariki.

Gavana Sanwo-Olu anaeleza : "Wenzangu wakazi wa Lagos, wakati tuna waombea waliojeruhiwa kupata afweni haraka, tunaridhika kusema hakuna ripoti ya vifo kama inavyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mashahidi wanasema milio ya bunduki ya hapa na pale imekuwa ikisikika mjini Lagos leo asubuhi.

Mashahidi karibu wanne wanasema wanajeshi walifyatua risasi na kuwaua takriban watu wawili. Lakini hadi hii leo hakuna ripoti za idadi ya watu waliofariki ingawa vídeo kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha miili ya watu barabarani.

Jeshi la Nigeria linakanusha ripoti hizo kwamba wanajeshi waliwashambulia kwa risasi waandamanaji likieleza ni habari za uongo.

Gavana Sanwo-Olu alitangaza amri ya kutotoka nje kwa muda usiojulikana ili kuzuia maandamano yaliyokuwa yakienea kwa wiki mbili sasa kutaka mageuzi katika idara ya polisi na kuvunjwa kabisa kikosi kinachodai kutenda ukatili dhidi ya wakazi, maarufu kama SARS.

Kikosi cha SARS kilivunjwa na serikali hapo Oktoba 11 lakini vijana wanaendelea kuandamana wakitaka mageuzi kamili.

Mji wa Lagos ulikuwa karibu mtupu Jumatano wakati polisi walikuwa wanaweka vizuizi kwenye njia kuu za mji huo.

Isah Aliu mkazi wa Lagos kama wakazi wenzake wanataka serikali kuu kuingilia kati na kufanya mgeuzi.

Aliu, Mkazi wa Lagos, anasema : "Vijana kwa hakika wamekasirishwa, na hivyo nina iomba serikali kuu kufanya kila iwezalo kutanzua tatizo hili na kmruhusu rais kulihutubia taifa ili utulivu uweze kurudi. Sisi vijana si wavivu tunaajribu kufanya kazi kwa bidii ili kujikimu kimaisha.

Wasanii mashuhuri wa Nigeria wameungana na vijana wanaotaka mageuzi na mchezaji wa kimataifa wa kandanda wa timu ya Manchester United Odion Ighalo alilaani shambulio hilo kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Ighalo, mchezaji kandanda wa Man United aeleza masikitiko yake : "Nimesikitishwa na yanayotokea, siwezi tena kunyamaza kimya na yanayo tendeka nyumbani. Kwa serikali kupeleka wanajeshi barabarani kuwaua raia wake wenyewe, raia wanaoandamana kwa amani kutetea haki zao, si jambo linalokubalika.

Mgombea kiti cha urais hapa Marekani Joe Biden amemhimiza rais wa Nigeria na jeshi la nchi hiyo kuwacha kuwabana waandamanaji. Katika tarifa yake amesema ni lazima Marekani isimame pamoja na Wanigeria wanaoandamana kwa amani kutaka mageuzi katika idara ya polisi na kukomesha ulaji rushwa.

Madai ya waandamanaji yamongezeka kutoka mageuzi ya polisi hadi mageuzi muhimu ya utawala ili kupambana na rushwa katika taifa lenye wakazi wengi barani Afrika.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG