Kuondolewa kwa Bazoum Niger ni hatari kwa demokrasia na usalama wa bara la Afrika asema mshauri wake

Maafisa wa jeshi wakiwasili Accra, Ghana Agosti 17, 2023. Picha na REUTERS/Francis Kokoroko.

Iwapo wanajeshi waloasi, waliomuondoa madarakani Rais wa Niger Mohamed Bazoum, watafanikiwa na mapinduzi yao, basi jambo hilo litasababisha kitisho kikubwa kwa demokrasia na usalama katika kanda ya Afrika Magharibi na bara zima la Afrika kwa ujumla.

Ameonya afisa wa ngazi ya juu wa chama cha kisiasa cha Bazoum wakati wa mahojiano na Shirika la habari la Associated Press.

Naibu katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Ujamaa cha Niger, Boubacar Sabo, alisema Bazoum "alitekwa nyara" na wanajeshi ambao ni walinzi wa rais waliompindua Julai 26 na tangu wakati huo wamemuweka kizuizi nyumbani kwake.

"Kinachotokea Niger, kama kitafaulu, ni mwisho wa demokrasia barani Afrika. Demokrasia Imekwisha.... Ikiwa tutapigana, itakuwa kuzuia mambo kama hayo kutokea na kuhakikishia mustakabali mzuri wa bara letu," alisema Sabo Alhamisi.

Katika kanda hiyo lililojaa mapinduzi ya kijeshi, Niger inachukuliwa kuwa ni moja ya nchi ya mwisho kuwa na demokrasia ambayo mataifa ya Magharibi yangeweza kushirikiana nayo ili kukomesha uasi wa wanamgambo wakislamu unaoongezeka ambao unaohusishwa na makundi ya al-Qaida na Islamic State.

Kupinduliwa kwa rais Bazoum takribani mwezi mmoja uliopita ni pigo kubwa kwa Marekani, Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya, ambayo yamewekeza mamilioni ya dola kama msaada wa kijeshi kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa jeshi la Niger na - kwa Wafaransa – kuendesha operesheni za pamoja za kijeshi.

Kamati ya Wakuu wa Majeshi ya ECOWAS mjini Accra. Agosti 17, 2023. Picha na REUTERS/Francis Kokoroko.

Tangu jeshi kunyakua mamlaka, katika kile ambacho wachambuzi na wenyeji wanasema kilichochewa na mzozo wa ndani kati ya Bazoum na mkuu wa walinzi wa rais, kiongozi mpya Jenerali Abdourahmane Tchiani, anaonekana akitumia malalamiko ya wananchi dhidi ya utawala wa kikoloni, Ufaransa na kuunyamazisha upinzani ili kupata umashuhuri zaidi.

Hata hivyo, Sabo, ni mmoja kati ya wakosoaji wachache wa serikali ya kijeshi ambao bado wako nchini bila ya kwenda mafichoni.

Sabo anasema kwamba, mawaziri kadhaa na wanasiasa wa ngazi za juu wamewekwa kizuizini huku wanaharakati wa mashirika ya kutetea haki za binadamu wakisema hawawezi kuwafikia, na wengine wakikabiliwa na vitisho.

Anasisitiza kwamba namna serikali inayoungwa mkono katika mji mkuu haimuliki umaarufu wao, kwa sababu serikali ya kijeshi imekuwa ikiwalipa watu kufanya mikutano ya hadhara kwa niaba yake. Mji wa Niamey pia haujapata kua ngome ya Bazoum, hivyo Baraza la Kijeshi limechukua fursa hiyo kujiimarisha, alisema.

Mikutano ya watu wanaoliunga mkono Baraza la Kijeshi imekuwa ikifanyika karibu kila siku ikiwa na mamia ya watu, na wakati mwingine maelfu ya watu wakiandamana barabarani, wakipiga honi za magari na kupeperusha bendera za Niger na Rashia na kuimba “Ufaransa iondoke." Baraza la kijeshi limefuta makubaliano kadhaa ya kijeshi na Ufaransa na kuomba msaada kutoka kwa kundi la mamluki la Wagner la Russia.