Idadi ya kesi zilizothibitishwa za virusi vya corona kote duniani zimeongezeka na kufikia milioni 4.
Wakati huo huo baadhi ya nchi ambazo zimepigwa vibaya na janga hili zikijitayarisha kwa awamu nyingine ya hatua kali licha ya khofu kutanda kuhusu wimbi la pili la maambukizi.
Idadi ya kesi zilizothibitishwa za virusi vya corona kote duniani zimeongezeka na kufikia zaidi ya milioni nne huku baadhi ya nchi ambazo zimepigwa vibaya na janga hili zikijitayarisha kwa awamu nyingine ya hatua kali licha ya khofu kutanda kuhusu wimbi la pili la maambukizi.
Wakati janga hilo likisababisha athari kubwa za kiuchumi kuwahi kuonekana tangu kipindi kibaya cha kudorora kwa uchumi katika miaka ya 1930 na kusababisha mamilioni ya watu kukosa ajira, serikali zinajaribu kudhibiti kusambaa kwa COVID-19 huku zikijitahidi kujaribu kuondoa marufuku ya muda mrefu ya kutotoka nje na kuleta ahueni kwa uchumi wa mataifa yao.
Idadi ya vifo duniani ikiwa zaidi ya 279,000 na waliopona wakikaribia milioni 1.4, nchi pia zina hamu kubwa ya kuepuka wimbi la pili la maambukizi ambalo huenda likawa na athari kubwa kwa mifumo ya afya katika nchi zao.
Remdesivir
Wizara ya Afya na Huduma za Binadamu nchini Marekani imesema Jumamosi kuwa itaruhusu idara za afya za majimbo kugawa dawa ya Remdesivir iliyotengenezwa na kampuni ya Gilead Sciences ili kupambana na COVID-19, na Marekani itapokea kiasi cha asilimia 40 ya mchango kutoka kwa kampuni hiyo.
Gilead imeelezea nia yake ya dhati ya kutengeneza takriban dawa 607,000 katika kipindi cha wiki sita zijazo hapa nchini Marekani na kusema idara za afya katika majimbo ya Marekani zitaigawa dawa hiyo kwa mahospitali husika kwenye majimbo yao, taarifa ya wizara ya afya imesema.
Ijumaa Idara ya Marekani na Chakula na Madawa, FDA, imeotoa idhini ya dharura kwa dawa hiyo kupewa wagonjwa walioathiriwa vibaya na COVID-19, na hivyo kufungua njia kwa matumizi makubwa katika hospitali kote nchini. Takwimu zimeonyesha kuwa dawa hiyo imesaidia kupunguza muda wa kukaa hospitali kwa wagonjwa waliopata maambukizi.
Malaysia
Malaysia inajitahidi kuwapima mamilioni ya wahamiaji kubaini kama wana virusi vya corona ili kuepuka kurejewa kwa mlipuko ambao umeipiga nchi jirani ya Singapore, ambako wafanyakazi wa kigeni walisongamana katika mabweni na wengi wao walithibitishwa kuwa na COVID-19.
Wiki kadhaa baada ya janga kutangazwa, Singapore ilipongezwa kwa juhudi zake za kufuatilia maambukizi ya virusi kwa kuchukua hatua za mapema, na kuwaeleza raia kuhusu hatari za ugonjwa na kutumia njia ya ufuatiliaji wa karibu.
Katikati ya mwezi Aprili, milipuko katika mabweni ambayo hayakuwa na ufuatiliaji mkubwa ambako kulikuwa na maelfu ya wafanyakazi wahamiaji yalikumbwa na idadi kubwa ya kesi za virusi vya corona.
Taifa hilo dogo hivi sasa lina kesi nyingi za virusi vya corona katika eneo la Asia Kusini Mashariki, zaidi ya kesi 21,000. Malaysia ina kesi 6,535 ambazo zimethibitishwa na chini ya watu 1,000 ni miongoni mwa wahamiaji.
Kama ilivyo Singapore nchi hiyo inategemea kwa kiasi kikubwa ajira nafuu kutoka katika nchi za karibu ili kukidhi mahitaji ya wafanyakazi wa viwandani. Wengi wao wako katika mashamba ya mpira na mitende. Serikali inasema ina kiasi cha wahamiaji milioni mbili na nusu wanaoishi nchini humo kihalali, ingawaje kuna wengi ambao wako nchini kinyume cha sheria.
Zambia
Zambia imeomba mkopo kutoka shirika la Kimataifa la Fedha duniani, IMF, kwa ajili ya mapambano ya COVID-19, wakati taifa hilo likianza kuorodhesha washauri wa kifedha ambao watasaidia katika kushughulikia kupunguza mzigo wa madeni, wizara ya fedha ya nchi hiyo imesema hivi leo Jumapili.
Zambia tayari imegubikwa na ongezeko la deni la umma kabla ya mlipuko wa virusi vipya vya corona na kulazimisha kufungwa kwa shughuli mbali mbali kote ulimwenguni, na hivyo kuwa pigo kubwa kwa mahitaji ya mali ghafi.
Zambia ni mzalishaji wa pili kwa ukubwa wa madini ya shaba barani Afrika. Majadiliano ya IMF kuhusu mkopo wa haraka yanaendelea, taarifa ya wizara ya fedha imesema.
Imetayarishwa na mwandisi wetu Khadija Riyami, Washington, DC.