Mamlaka ya kilimo na chakula nchini humo, ikijibu madai ya serikali ya Tanzania kuwa haijapokea ithibati rasmi ya marufuku hiyo, imeeleza kuwa malori yaliopo katika mpaka wa Namanga hayata ruhusiwa kuingia Kenya hadi suala hilo lisuluhishwe, kama anavyoripoti mwandishi wetu wa Nairobi, Kennedy Wandera.
Kufuatia matamshi ya serikali ya Tanzania mwishoni mwa wiki kuwa haijapokea ithibati rasmi ya kupigwa marufuku mahindi yake kuingia Kenya kwa madai ya kuwa na viwango vya juu vya sumu vinavyoyafanya kutokuwa salama kwa matumizi ya binadamu, serikali ya Kenya inaeleza kuwa imefanya hivyo kwa sababu maisha ya raia wake ni muhimu mno kuliko kitu kingine.
Mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya Kilimo na Chakula, Kenya, Kello Harsama, ambaye ameiandikia mamlaka ya ushuru nchini Kenya kusimamisha mara moja uingizaji wa mahindi kutoka mataifa jirani ya Tanzania na Uganda, ameieleza VOA kuwa Kenya haiwezi kuchukulia kimzaha afya ya raia wake.
Mamlaka hiyo iliyo na majukumu ya kusimamia, kustawisha na kuendeleza kilimo na chakula nchini Kenya inaeleza kuwa hivi karibuni inatangaza mfumo na utaratibu mpya wa kuingiza chakula nchini Kenya. Na anayesajiliwa ni lazima apewe vyeti vya kuingiza chakula.
Jumamosi na Jumapili, misururu mirefu ya malori yaliobeba mahindi yalikataliwa kuingia Kenya kupitia mpaka wake na Tanzania eneo la Namanga, na Harsama anaeleza kuwa hayawezi kuruhusiwa Kenya hadi tatizo hili lipatiwe suluhu.
Hatua hii ya Kenya inatajwa kukiuka mkataba wa Jumuiya ya umoja wa Afrika Mashariki na itifaki ya soko la pamoja la jumuiya hiyo lakini si mara ya kwanza Kenya na Tanzania kujikuta hapa.
Mwaka 2017, serikali ya Tanzania iliwakamata na kuwapiga mnada zaidi ya ng’ombe elfu moja wa wachungaji wa Kenya walioripotiwa kuvuka mpaka na kuingia Tanzania na vile vile kuteketeza vifaranga zaidi ya elfu sita kutoka Kenya kwa madai ya kusambaza homa ya ndege nchini humo. Wakati huo serikali ya Kenya, iliishtumu Tanzania kwa kufanya hivyo bila kuieleza Kenya. Hatua hiyo ikizua mzozo wa kidiplomasia kati nchi hizi jirani.
Hata hivyo, Harsama anaeleza kuwa hatua hii ya kupiga marufuku uingizaji wa mahindi nchini mwake hauhusu Tanzania pekee na hivyo basi haliwezi kuwa suala la kidiplomasia.
Waziri msaidizi wa Kilimo nchini Tanzania Hussein Bashe amevieleza vyombo vya habari nchini humo kuwa hatua ya Kenya haikubaliki na inaenda kinyume na itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, afisa huyo wa Tanzania anaeleza kuwa hatua ya Kenya kwa kiasi kikubwa inakiuka uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania.