Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 06:53

Kenya yasema mgogoro wa usafiri wa anga na Tanzania umekwisha


Abiria wakiwa wamevalia barakoa safari za kimataifa ziliporejea uwanja wa Jomo Kenyatta, Nairobi, August 1, 2020.
Abiria wakiwa wamevalia barakoa safari za kimataifa ziliporejea uwanja wa Jomo Kenyatta, Nairobi, August 1, 2020.

Serikali ya Kenya imetangaza Jumamosi kuwa imefanya mazungumzo na Tanzania kusuluhisha mgogoro ulioibuka Ijumaa baada ya Tanzania kutangaza kusimamisha ndege za shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways (KQ) kufanya safari nchini humo.

Hatua ya Tanzania ilifuatia tangazo la serikali ya Kenya kutoiorodhesha nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi 11 ambazo wasafiri wake wanaruhusiwa kuwasili Kenya Jumamosi Agosti 1 wakati usafiri wa kimataifa unaporejea.

Waziri wa Uchukuzi nchini Kenya James Macharia wakati akizindua safari za kimataifa za Kenya Airways Jumamosi asubuhi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) ameeleza kuwa amefanya mazungumzo kupitia video na Waziri wa Kazi, Uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania Isack Aloyce Kamwelwe na kuzika mgogoro huo.

“Nimefanya majadiliano ya kina na mwenzangu kutoka Tanzania na kwa kweli hakuna mafarakano. Mwisho wa siku hii, ushauri uliotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Tanzania utabatilishwa na kuruhusu ndege za Kenya Airways kuingia Tanzania,” alieleza Macharia.

Waziri huyo ameeleza kuwa Kenya haijapiga marufuku ndege za Tanzania kuingia nchini mwake hata kama si miongoni mwa nchi 19 zinazoruhusiwa kuingia anga ya Kenya.

"Wasafiri kutoka Tanzania wanaweza kuja mapema hata leo. Hatujasimamisha ndege hizo. Hili suala dogo limetatuliwa na tunaamini kuwa ikiwa sio leo, kesho ndege zetu za Kenya Airways zitatua Tanzania, "alisema.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya safari za anga nchini Tanzania (TCAA), Hamza S. Johari alisema serikali ya Tanzania imesimamisha mara moja safari za ndege za shirika la Kenya Airways kutoka Nairobi kutua viwanja vyake vya ndege Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar mpaka siku patakapokuwa na taarifa mbadala.

Mpaka sasa serikali ya Tanzania haijatoa taarifa kuhusu matamshi ya Kenya.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Nairobi

XS
SM
MD
LG