Awali mwenyekiti CHADEMA, Freeman Mbowe alisema, kitendo cha kuenguliwa kwa wagombea wake wangeweza kuamua kususia uchaguzi huo, lakini amesema ni vyema kuingia katika ushindani wa kisiasa.
‘’Yote yaliyofanyika katika mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa, hatuna lugha nyepesi ya kutumia, bali kuelezea kuwa umekuwa ni ubakaji wa demokrasia, ulio wazi usio na chembe ya haya au aibu’’ amesema Mwenyekiti wa CHADEMA.
Mbowe alisema, licha wagombea wake kuenguliwa katika ngazi ya vijiji, wamebaki wagombea 4,175 kati ya vijiji 12,333, huku akisema kuwa wote waliobaki watajitahidi kupambana mpaka dakika za mwisho kukitetea chama chao.
Kwa upande wa chama cha ACT Wazelendo kupitia kwa aliyekuwa Mwenyekiti wake Zitto Kabwe, alisema kwa sehemu zote walizoenguliwa wanasheria wake wa chama wameshaelekezwa na kamati ya uongozi wa chama kufungua kesi za uchaguzi kila sehemu walizoenguliwa, huku akisema pale ambapo CCM wapo peke yake watapiga kura ya ’Hapana’.
‘Hatupaswi kukata tamaa, hata wangetubakizia katika kijiji kimoja, mtaa mmoja, kitongoji kimoja tungekwenda kushinda kwanza, halafu ndipo tuendelee na mapambano ya kuokoa huko kwingine,” alisema Zitto.
Chama tawala cha CCM, katika ufunguzi wa kampeni kimewasambaza baadhi ya viongozi wake wenye ushawishi katika mikoa yote nchini kama njia ya kuwaunga mkono wagombea wao katika uchaguzi huu utakaofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ambao ndio wasimamizi wa uchaguzi huu, wamesema kuwa jumla ya vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji 63,886 ndivyo vitakavyoshiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27.
Imetayarishwa na Egberth Alfred, Dar es Salaam, Tanzania