Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Januari 28, 2025 Local time: 06:22

Wachambuzi Tanzania wasema Trump utasaidia kumaliza vita duniani


Mgombea uchaguzi wa chama cha Republikan Donald Trump alipokuwa jukwaani kufuatia matokeo ya awali ya uchaguzi huko Florida Novemba 6, 2024. Picha na REUTERS
Mgombea uchaguzi wa chama cha Republikan Donald Trump alipokuwa jukwaani kufuatia matokeo ya awali ya uchaguzi huko Florida Novemba 6, 2024. Picha na REUTERS

Baada ya Donald Trump kutangazwa kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Urais nchini Marekani wachambuzi wa siasa na wasomi nchini Tanzania wamesema ushindi huo unaweza kusaidia kumaliza migogoro ya kivita katika maeneo mbalimbali duniani

Pia kuleta ahueni ya uchumi, kutokana na ahadi zake za kuhitimisha vita hivyo, huku wakizitaka nchi za Afrika kujifunza kutokana na uchaguzi huo.

Wachambuzi wa siasa nchini Tanzania wanasema ushindi huo umetokana na sera za Donald Trump zilizojikita katika kumaliza migogoro ya kivita, kupunguza ushuru pamoja na kupunguza wimbi la wahamiaji ambapo Rais huyo mteule aliahidi kuwahamisha wahamiaji wasiokuwa na vibali nchini humo.

Dkt Dotto Bulendu Mhadhiri kutoka Chuo cha Mtakatifu Agustine Mwanza amesema wananchi wa Marekani wamemchagua Donald Trump wakiamini kuwa atakwenda kuusimamisha uchumi wa Marekani na kuendelea kuifanya Marekani kuwa Taifa lenye nguvu Duniani kutokana na sera zake za ndani.

Wafuasi wa Donald Trump wakiwa nje ya bustani ya Madison Square huko New York wakati wa mkutano wa hadhara
Wafuasi wa Donald Trump wakiwa nje ya bustani ya Madison Square huko New York wakati wa mkutano wa hadhara

“Wamarekani wanaona watapata kiongozi ambaye hata tanua sana mbawa zake nje ya Taifa la Marekani na atatumia nguvu nyingi sana ndani ya marekani kitu ambacho kwa nje kina tafsiri yake kwamba kuna hofu labda misaada ya Marekani kwenda nje itapungua, ndani wanamuona Trump ni mtu ambae anakuja kuijenga upya na anakuja kuifanya marekani kubaki kuwa Taifa lenye nguvu duniani”. alisema Dkt. Bulendu.

Wachambuzi wanasema kuwa Mataifa ya Afrika yanaweza kujifunza umuhimu wa demokrasia thabiti, ushirikishwaji wa wananchi, na nguvu ya taasisi huru kutokana na uchaguzi wa Marekani na hivyo mataifa hayo yanapaswa kumilikisha mamlaka kwa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka.

Buberwa Kaiza Mchambuzi wa masuala ya Siasa kutoka Dar es Salaam amesema nchi za Afrika zinapaswa kujifunza namna ya kuendesha chaguzi zao kwa uhuru na uwazi kwa kuzingatia Demokrasia kutokana na uchaguzi huo hasa kwa kuzingatia muda unaotumika mpaka utangazaji wa matokeo.

“Nchi nyingi za Kiafrka utaona uchaguzi unafanyika wakisikia fulani kashindwa basi watazuia matokeo kutangazwa watafanya vurugu kidogo watu hawatulii mpaka apitishwe wanaemtaka hata kama hajashinda kwahiyo unaona kabisa kwa wenzetu wa Marekani wanajua kabisa watu ndio wanaofanya maamuzi na wakishafanya maamuzi hakuna watu wengine na ndio maana matangazo ya kura yanafanyika mapema sana”. alisema Kaiza

Hata hivyo Mbwana Aliyamtu Mchambuzi wa Siasa kutoka Arusha amesema iwapo Rais Mteule Donald Trump atashugulikia migogoro ya kivita inayoendelea maeneo mbalimbali itasaidia kuleta ahueni ya uchumi kwenye bara la Afrika na kupunguza bei ya bidhaa mbalimbali ambazo zilipanda bei kutokana na vita hivyo.

“Siasa ya Marekani inaathiri dunia nzima Trump atakapoapishwa na kuchukulia hatua vita inayoendelea Ukraine na Gaza na kusitisha mapigano kimsingi itapunguza ukali wa uchumi wa dunia maana yake pia Afrika itapata nafuuu maana bei za mafuta zitashuka bei ya bidhaa pia kama ngano ambayo imekuwa ikitegemewa sana kutoka katika nchi za Russia na Ukraine”, alisema Aliyamtu.

Donald Trump ameshinda na kuchaguliwa kuwa Rais wa 47 wa Marekani dhidi ya Mpinzani wake Kamala Harris, kwa ushindi huo Rais huyo anaweka rekodi ya kuwa Rais aliyewahi kushindwa uchaguzi na baadae kushinda katika uchaguzi unaofuata.

Forum

XS
SM
MD
LG