Your browser doesn’t support HTML5
Iran ilirusha zaidi ya darzeni moja ya makombora ya masafa mafupi siku ya Jumnanne usiku katika makambi mawili ya kijeshi ya Iraq ambayo ni kituo kinachotumiwa na wanajeshi wa Marekani.
Tehran inaeleza kwamba mashambulizi hayo ni ulipizaji kisasi mauaji ya Jenerali Qassem Soleimani yaliyofanywa na Marekani karibu na Baghdad siku ya Ijuma.
Rais Trump
Muda mfupi tu baada ya mashambulio hayo jana usiku Rais Donald Trump alikutana na washauri wake wa usalama na kutoa ujumbe wa tweeter akithibitisha shambulio hilo kwa kusema kwamba“Tathmini inafanyika hivi sasa. Hadi sasa mambo ni shuwari” Nitalihutubia Taifa kesho.”
Wizara ya Ulinzi ya Marekani
Maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wamesema Jumatano kwamba baada ya tathmini hakuna majeruhi miongoni mwa wanajeshi wa Marekani kufuatia mashambulio hayo ya Iran katika makambi ya jeshi la anga la Iraq la al-Asad, na Irbili.
Kwa upande wake kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akilihutubia taifa Jumatano, amesema mashambulio ya makombora kutokea Tehran dhidi ya vituo vya Marekani nchini Iraq ni ‘kofi la uso’ kwa Marekani na inabidi iondoshe majeshi yake kutoka kanda zima la Mashariki ya Kati.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif ameonya kwamba ikiwa Marekani itachukua hatua zaidi, basi Iran itajibu kwa namna inayostahili.
"Tumeshaeleza bayana kwamba ikiwa Marekani itachukua hatua zaidi, Iran itajibu kwa namna inayostahili na kwa vikali zaidi". amesema Zarif
Umoja wa Ulaya umetoa wito Jumatano kutaka usitishaji mara moja wa utumiaji silaha za hatari katika ugomvi wa Mashariki ya Kati katika uhasimu uliopo kati ya Marekani na Iran, na kuzihimiza pande zote mbili kuanza majadiliano.
Umoja wa Ulaya
Rais wa Kamisheni ya EU, Ursula von der Leyen akizungumza na waandishi habari mjini Brussels amesema ana tarajia kujadili hali hiyo na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson watakapokutana mjini London Jumatano mchana.
"Ninataka kusisitiza kwamba matukio ya hivi sasa huko Iran na IraQ na kanda zima yanaleta wasi wasi mkubwa. Kitu kimoja kilicho bayana, hali ya hivi sasa inahatarisha juhudi za miaka ya hivi karibuni na yatakua na athari katika juhudi muhimu za kupambana na ISIS." amesema Leyen
Wachambuzi wanasema kutokana na kutokuwepo na majeruhi miongoni mwa Wamarekani ni ishara kwamba Iran imekusudia kutoa onyo tu kwa Marekani kwamba inaweza kujibu vikali.
Baraza la Atlantic
Thomas Warrick wa Baraza la Atlantic anaiambia Sauti ya Amerika kwamba huenda huu ulikua uamuzi wa makusudi wa Iran.
Hivyo inaonekana kana kwamba Iran imechagua kujibu kwa makombora ya masafa mafupi ili kutoa ujumbe maalum. Walijaribu kulipiza kisasi, lakini kwa njia ambayo wanadhibiti hali ya mambo kuliko kumtumia mmoja wapo ya washirika wake kutekeleza mashambulio hayo. Na ni wazi walitaka kupeleka ujumbe bayana kwamba wana uwezo wa kujibu vikali," amesema Warrick
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.