Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:26

Iraq : Iran yashambulia kambi mbili yalipo majeshi ya Marekani


Kituo cha jeshi la anga cha Al-Asad nchini Iraq
Kituo cha jeshi la anga cha Al-Asad nchini Iraq

Iran imeshambulia kwa kutumia darzeni ya makombora ya balistika mapema siku ya Jumatano ikilenga kambi mbili za jeshi la anga nchini Iraq ambazo zinakaliwa na vikosi vya jeshi la Marekani, Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeeleza.

Rais wa Marekani Donald Trump alituma ujumbe wa tweet masaa kadhaa baadae kuwa tathmini juu ya vifo na uharibu uliotokana na shambulizi hilo unafanyika, lakini "hadi hivi sasa kila kitu kiko shuwari.”

“Sisi tunazo silaha zenye nguvu zaidi na jeshi lililokuwa na vifaa vya kutosha kuliko nchi yoyote duniani, kwa kiwango kikubwa! alisema Trump.

Trump alikutana na timu yake ya usalama wa taifa ndani ya White House, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo na Waziri wa Ulinzi Mark Esper. Alikuwa amepanga kutoa tamko Jumatano asubuhi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema katika ujumbe wake wa tweet kuwa Iran ilichukuwa hatua hiyo na imekamilisha “kiwango stahili cha kujihami” kwa kuilenga kambi “ambako shambulizi la kiuoga dhidi ya raia wetu na maafisa wetu wa ngazi ya juu lilifanyika.”

“Hatutaki kuongeza mapambano ya kivita, lakini tutajitetea dhidi ya uvamizi wowote utakaofanyika,” Zarif alisema.

Shambulizi la makombora ni hatua mpya katika mlolongo wa matukio ya kipindi cha wiki mbili zilizopita na kuongeza mvutano kati ya Marekani na Iran.

Marekani ilikilaumu kikundi cha wanamgambo kinachosaidiwa na Iran kwa shambulizi la roketi katika ardhi ya Iraqi lililouwa mkandarasi wa jeshi la Marekani.

Kufuatia hilo mashambulizi ya Marekani yalilenga maeneo ya wanamgambo nchini Iraq na Syria, na kusababisha malalamiko yaliyotolewa na serikali ya Iraq na kufuatiwa na maandamano yaliyoongozwa na wanamgambo katika Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad.

Siku ya Ijumaa, shambulizi la anga lililofanywa na Marekani lilimuua Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi maalum cha Quds karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilisema makombora yaliyorushwa na Iran yalilenga kambi ya Al-Asad, iliyoko takriban kilomita 60 magharibi ya Baghdad, na pia kambi nyingine ya Irbil, ambayo iko katika eneo la Iraq la mkoa wa Wakurdi wanaojitawala.

XS
SM
MD
LG