Jengo la kihistoria Bait al-Ajaaib laanguka Zanzibar

Jengo la ghorofa maarufu Bait al-Ajaaib. Picha kwa hisani ya Global Publishers TV, Tanzania.

Jengo la ghorofa linalo fahamika kama House of Wonders (Bait al- Ajaib) lililopo Stone Town, Zanzibar limeanguka Ijumaa huku baadhi ya watu walio kuwemo wakidaiwa kufukiwa na kifusi cha jengo hilo. 

Jengo hilo linalo tazamana na Bustani ya Forodhani ni jengo kubwa na refu zaidi katika eneo la Stone Town na ni miongoni mwa majengo ya zamani yaliyo jengwa mwaka 1883 na baadaye kufanyiwa ukarabati miaka ya karibuni.

Taarifa kutoka katika eneo la ajali hiyo zinasema kuwa wafanya kazi wanne wamefunikwa na kifusi wakati juhudi za uokoaji zikiendelea.

Rais wa Zanzibar Hussein Mwinyi alifika katika eneo la tukio ambapo alipewa taarifa juu ya juhudi za uokoaji zinazo endelea katika jengo hilo la kihistoria.

Vyanzo vya habari vinaeleza kuwa jengo hilo ambalo liko pembezoni mwa Bahari ya Hindi katika Barabara ya Mizingani, limejengwa kati ya makumbusho ya kale ya Zanzibar ambalo pia limekuwa kielelezo kikubwa cha historia na tamaduni za watu wa Zanzibar na kukua kwa lugha ya Kiswahili.

House of Wonders lilikuwa miongoni mwa majengo sita ya Ikulu na makazi ya zamani ya Sultan wa pili wa Zanzibar, Barghash bin Said, enzi za ukoloni na biashara, katika karne ya 17.

House of Wonders kwa sasa lilikuwa limefungwa kutumika kutokana na sehemu kubwa ya jengo hilo kupasuka na kuharibika na kuanguka roshani yake mwaka 2012 kisha kuanguka paa la jengo hilo mwaka 2015.

Na hivyo kuharibu muundo, uimara na muonekano wa jengo hiloambapo makumbusho yake yalilazimika kuhamishiwa eneo jingine.

Kulingana na Global TV Online Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini, Magharibi, Alhaji Awadhi, hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo. Msaidizi wake amesisitiza ni mamanda pekee anayeweza kuzungumziasuala hilo.