Je, kauli ‘udhaifu huo utarekebishwa’ ni sawa na ‘bunge ni dhaifu’?

Rais John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa na watendaji wakuu wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mussa Assad kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Professa Mussa Assad Machi, 2016.

Zimebakia siku tisa ambapo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mussa Assad, anatarajiwa kujitetea mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa tuhuma za kuudhalilisha mhimili huo.

Spika Ndugai kupitia vyombo vya habari wiki iliyopita alimtaka Mussa Assad, CAG afike mwenyewe kwa hiyari yake mbele ya kamati ya maadili ya Bunge tarehe 21. 01.2019, vingenevyo atapelekwa kwa pingu.

Isemavyo mitandao ya kijamii

Kumekuwa na hisia mseto tangu Spika atangaze CAG atahojiwa juu ya kauli yake kuwa “udhaifu huo utarekebishwa.” Baadhi ya wana mitandao ya kijamii nchini Tanzania wanaamini kuwa kusema hivyo hakumaanishi kuwa bunge ni dhaifu.

Wachangiaji wengine wamesema kuwa kuna tofauti kati ya kusema "huo ni udhaifu na bunge ni dhaifu."

Baadhi ya wachangiaji hao wanaamini kuwa kauli ya CAG katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kuwa “Bunge halifanyi kazi yake kama linavyotakiwa na kwamba ni matarajio yake kwamba udhaifu huo utarekebishwa,” ilikuwa ina onyesha mapungufu yaliyo kuwepo ndani ya Bunge na wala huko hakumaanishi kuwa bunge ni dhaifu.

Katika mahojiano hayo Profesa Assad alikuwa akijibu swali kuhusu kutotekelezwa kwa mapendekezo anayotoa kwenye ripoti zake, hasa kuhusu ufisadi.

Alichosema Profesa Assad

“Kama tunatoa ripoti na kuna ubadhirifu na hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa lisimamie na kuhakikisha kwamba pale penye matatizo, linahakikisha kuwa hatua zinachukuliwa. Sasa, sisi kazi yetu ni kutoa ripoti tu,” alijibu.

“Na huo udhaifu, nafikiri ni jambo la kusikitisha, lakini ni jambo ambalo tunaamini muda si mrefu litarekebishika. Lakini tatizo kubwa tunahisi kwamba Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa. Na sitaki kuwa labda nasema jambo hili kwa sababu linahusisha watu fulani, hapana. Lakini nafikiri Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata udhaifu ambao unaonekana, utakwisha.

Ndugai, Assad wakosolewa

Wale wanao mkosoa Profesa Assad kupitia mitandao ya kijamii wanadai kuwa kiongozi mwenye dhamana ya uongozi anatakiwa ajue kipi useme wapi au kipi usiseme.

Baadhi wamesema kuwa Profesa Assad alisema kwa ujasiri kile anacho simamia bila ya uoga, lakini wanamkosoa kwa kutotumia diplomasia na kuheshimu mihimili mingine.

Lakini ukosoaji huo pia ulielekezwa kwa Spika wa Bunge la Muungano Job Ndugai. Wanasema kwa kutambua unyeti wa CAG naye alipaswa kuepuka baadhi ya kauli za udhalilishaji dhidi ya CAG.

Hata hivyo gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limeeleza kuwa kitendo hicho kitamfanya Profesa Assad aandike historia ya kufikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya kamati hiyo tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo Disemba 1, 2014.

Spika Ndugai

Alipoulizwa kuhusu suala hilo Ijumaa, Spika wa Bunge, Job Ndugai aliiambia Mwananchi kuwa hawezi kuzungumzia maoni hayo yaliyo kwenye ripoti hizo mbili hadi hapo Profesa Assad atakapohojiwa Januari 21, lakini akasema anao ushahidi wa maandishi kuthibitisha kuwa chombo chake kinatekeleza wajibu kilichopewa na umma.

Mwenyekiti wa LAAC

Mwenyekiti wa Laac, Vedasto Mwiru hakutaka kuzungumzia suala hilo alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mapendekezo yaliyo kwenye ripoti hizo, hadi sakata hilo litakapoisha.

Mbunge Zitto Kabwe

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, ambaye aliwahi kuiongoza PAC, alisema kusuasua kwa utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti za CAG ni kikwazo kwa CAG.

“Hizo takwimu zinathibitisha maneno na manung’uniko ambayo CAG amekuwa nayo,” alisema.

“CAG si polisi wala si Takukuru. Wanaopaswa kufuatilia utekelezaji wa hayo mambo ni Bunge kupitia kamati zake. Kwa hiyo kama kamati hazifanyi kazi CAG atakuwa anaandika ripoti tu,” alisema.

Kiongozi huyo wa Chama cha ACT alitetea kauli aliyotoa Profesa Assad katika mahojiano hayo na kituo cha UN.

'“CAG hakusema Bunge ni dhaifu, alisema ni udhaifu wa Bunge. Kwa hiyo Spika amechukua hatua kwa jambo ambalo ni maoni tu,” alisema.

Muhtasari wa Ripoti za CAG

Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi baadhi ya ripoti za CAG zinaweza kuwa ndizo zilizo mfanya Profesa Assad atoe maoni hayo kuwa Bunge halitekelezi wajibu wake ipasavyo.

Hadi sasa, Profesa Assad ameshatoa ripoti mbili na katika utangulizi wa ripoti hizo zote (ya mwaka 2015/16 na ya 2016/17), ameeleza kutoridhishwa kwake na utekelezaji wa maoni ya ukaguzi, akibainisha baadhi ya mambo ambayo kamati za Bunge (ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) na Hesabu za Serikali (PAC), zilitakiwa kuyafanyia kazi baada ya kuzipokea.