Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:00

Naibu Spika aitaka Chadema kuleta ushahidi bungeni


Mbunge Peter Msigwa
Mbunge Peter Msigwa

Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini nchini Tanzania, Peter Msigwa (Chadema) ametakiwa kuwasilisha nyaraka zinazodai kuwa na habari mbaya za rushwa katika Mkataba wa Makubaliano (MoU) juu ya utengenezaji wa pasipoti za kielektroniki uliozinduliwa hivi karibuni.

Msigwa amesema bungeni Ijumaa kuwa chama chake cha Chadema, kimepata nyaraka zinazoonyesha gharama ya pasipoti za kielektroniki ambayo ilizinduliwa na Rais John Magufuli, hazikufuata taratibu za ununuzi wa haki.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini Tanzania wakati wa uzinduzi wa pasipoti za kielektroniki, serikali ilibainisha kuwa hati hizo zitatolewa kwa gharama ya Sh 150,000 ambazo zitadumu kwa miaka 10.

Mradi wa pasipoti za kielekroniki unatekelezwa na Ireland na Kampuni HID ya Marekani kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 57.82.

Naibu Spika wa Bunge, Dkt Tulia Ackson amemwagiza Msigwa kuleta nyaraka hizo bungeni.

Msigwa aliibua suala la mradi huo wakati wa kujadili taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika kipindi cha Januari 2017 hadi Januari 2018.

“Wakati mfumo huu unazinduliwa, hatukuambiwa ikiwa ni pasipoti za kielektroniki au uhamiaji. Umma unahitaji kuambiwa kipi ni kipi. Tunahitaji ufafanuzi kwenye suala hili,” alisema.

Tuhuma hizo zilimfanya Naibu Spika, Dkt Ackson kuingilia kati na kumtaka mbunge huyo kupeleka nyaraka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge yenye uwezo wa kuchunguza na kutoa ushauri hatua gani zichukuliwe kuhusu jambo hilo.

Hivi karibuni, Idara ya Uhamiaji ilibainisha ufisadi wa Sh bilioni 400, zilizolengwa kuhujumiwa kupitia zabuni ya utengenezaji wa pasipoti mpya za kielektroniki za kusafiria.

Pia lilibainisha hujuma mpya ya kuwepo kwa kundi la wanasiasa linalotumiwa kufanya siasa chafu za kudhoofisha mchakato wa utoaji hati mpya za kielektroniki za kusafiria na kuwataka kuacha kufikiria maslahi yao na kutanguliza mbele maslahi ya Taifa.

XS
SM
MD
LG