Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 00:17

Tutamlazimisha Kenyatta kuheshimu katiba, asema Miguna Miguna


Mwanaharakati wa Kenya Miguna Miguna.
Mwanaharakati wa Kenya Miguna Miguna.

Mwanaharakati na mwanasiasa wa Kenya Miguna Miguna ambaye alilazimishwa kwenda uhamishoni nchini Canada, alisema Ijumaa kwamba hataruhusu utawala wa rais Uhuru Kenyatta "kwendelea kutoheshimu sheria za Kenya."

Katika mahojiano ya moja kwa moja na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, Miguna alisema kwamba mawakili wake tayari walikuwa wamewasilisha kesi katika mahakama moja mjini Nairobi kushinikiza serikali ya nchi hiyo kurejesha cheti chake cha kusafiria na vile vile kumruhusu kuingia nchini.

"Hatutakubali...Tutamlazimisha Uhuru kuheshimu katiba," alisema kwa njia ya simu kutoka nyumbani kwake mjini Richmond Hill, Ontario, Canada.

Aidha, Miguna alisema kwamba hatapumzika hadi pale serikali ya Uhuru Kenyatta itakapokubali kwamba haiko mamlakani kwa njia halali.

"Uhuru ni lazima aamue kama anataka kuongoza kwa mujibu wa katiba au la," alisema Miguna.

Alipoulizwa kama ana imani kwamba uamuzi utakaotolewa na mahakama juu ya suala hilo utaheshimiwa na serikali licha ya kutofanya hivyo hapo awali baada ya kuamriwa wawafikishe mahakamani watuhumiwa, Miguna, ambaye pia ni mwanasheria, alisema hawezi kulijibu swali hilo kwa sababu bado hatua hiyo haijafikiwa.

Alitaka uchaguzi mpya wa urais ufanyike kabla ya mwezi Agosti. Miguna amesema kamwe hakuukana uraia wa Kenya na kwamba ana uraia pacha, ambao unnampa haki zote za raia wa nchi hizo mbili.

Kiongozi wa muunganio wa National Super Alliance (NASA), Raila Odinga, alisema Jumatano kwamba angependa uchaguzi ufanyike mwezi Agosti. Miguna hata hivyo, alikuwa na maoni tofauti.

"Hata mwezi mmoja unatosha kufanya maageuzi ya mfumo wa uchaguzi yanayohitajika," alieleza Miguna.

Miguna aliwasili nchini Canada Jumatano usiku baada ya kuondoshwa kwa lazima nchini Kenya, ambako alikuwa anakabiliwa shtaka la uhaini.

Alisema kwamba atawasilisha malalamiko mengine kwenye mahakama kuhusu kuharibiwa kwa nyumba yake na maafisa wa polisi waliomkamata.

Kwa mujibu wa Miguna, maafisa waliokuwa na mavazi ya binafsi waliingia nyumbani kwake katika mtaa wa Runda wiki ilityopita na kutumia vilipuzi ili kumfikia kwenye chumba alimokuwa.

Baadaye alipelekwa kwenye vituo kadhaa vya polisi na kufikishwa katika mahakama moja mjini Kajiado, takriban kilomita 80 kutoka mjini Nairobi, siku ya Jumanne.

Wakati wa mahojiao ya Ijumaa, Miguna alisema kwamba licha ya kumkosoa vikali Raila Odinga na kusema kuwa hana uwezo wa kuiongoza Kenya, sasa amebadilisha msimamo.

"Haya hufanyika duniani kote. Ninajua Raila si malaika lakini hata Barack Obama alikuwa hasimu mkubwa wa Hillary Clinton na baadaye walifanya kazi pamoja."

Kuhusu uraia pacha, mwanasheria huyo alisema hakuna mtu yeyote ambaye anaweza "kuninyang'anya uraia wa Kenya."

Alisema polisi wa Kenya walikiuka sheria kwa kumuondoa kwa nguvu nchini.

Kuhusu vuguvugu la NRM, Miguna alisema kuwa bado yeye ni Jenerali wake lakini haliwezi kufutiliwa mbali kwa sababu halijasajiliwa.

XS
SM
MD
LG