Japan yalazimika kuteua wafanyakazi wapya kutokana na China kuongeza harakati zake karibu na Taiwan

Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida afanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.

China imeongeza harakati za kijeshi karibu na Taiwan na Japan imeanza kufanya mabadiliko katika misimamo ya wafanyakazi wa serikali hiyo.

Japan ilitangaza uteuzi wa nafasi mbili muhimu za jeshi la ulinzi wiki iliyopita. Wachambuzi wanadhani kuwa hatua hiyo inaashiria kuongezeka kiwango cha umuhimu ambao Tokyo inaipa hadhi ya eneo la mlango wa bahari la Taiwan.

“China imekuwa ikikabiliana na harakati nyingi za uchokozi zinazoendelea karibu na Taiwan na wananchi wa Japan wana wasiwasi mkubwa kuhusu hali hii,” Stephen Nagy, mtaalam wa usalama wa kikanda katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kikristo nchini Japan, ameiambia VOA katika mahojiano ya simu.

“Japan imetuma ujumbe kwa Beijing kuwa inataka kutoa kipaumbele cha amani na uthabiti katika eneo lote la mlango wa bahari la Taiwan kwa kuwateua watu ambao ni waungaji mkono wa Taiwan katika nafasi zinazohusiana na ulinzi,” alisema.

Vyombo vya habari kadhaa vimeripoti wiki iliyopita kuwa Japan imemteua afisa anayehudumu katika wizara ya ulinzi kuwa mwambata kijeshi wa Taiwan, ikibadili sera yake ya zamani ya kuteua maafisa wa jeshi la Ulinzi wa Japan waliostaafu kutumikia nafasi hiyo katika Jumuiya ya Mawasiliano kati ya Japan na Taiwan, taasisi inayowakilisha maslahi ya Japan huko Taipei.

Wataalam wanasema kuwa hatua hii inaonyesha azma ya Tokyo katika kuboresha kiwango cha mawasiliano kuhusiana na hali ya usalama katika eneo lote la pwani ya Taiwan. Wana matumaini kufanikisha lengo hilo kwa kumteua mtu anayefaa kuwa ndiye muambata wa ulinzi.

“Hatua hii inaeleza juu ya uwezo wa kuanzisha uhusiano wenye nguvu zaidi katika ngazi ya kibinadamu,” Alessio Patalano, profesa wa masuala ya vita na mikakati huko Asia Mashariki katika Chuo cha Kings College, London, aliiambia VOA katika mahojiano ya simu.

“Uthabiti katika mlango wa bahari wa Taiwan unaathari zisizo zuilika kwa usalama wa Japan na kuna ongezeko la ufahamu mjini Tokyo kwamba kuwa na mtu Taipei inawawia wepesi kuwa na mazungumzo yenye ubora zaidi,” alisema.

Na juu ya uteuzi huu mpya wa muambata wa ulinzi huyu huko Taiwan, ni uteuzi pia uliofanywa na Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida wa Minoru Kihara, mwanasiasa ambaye ana uzoefu wa kushawishi uhusiano bora kati ya Tokyo na Taipei, kama Waziri mpya wa Japan wa Ulinzi. Uteuzi wa Kihara ni sehemu ya mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyotangazwa na serikali ya Japan Septemba 13.

Kihara alikuwa katibu mkuu wa kikundi cha wabunge wa pande mbili Japan na Taiwan na alizuru Taiwan kama ni sehemu ya ujumbe wa wabunge wa Japan mwezi Agosti.