Jeshi la Ulinzi la Israel lilisema mashambulizi hayo yamewalenga wanamgambo eneo la kaskazini la Shati na pia huko Khan Younis.
Vikosi vya Israeli viliuwa darzeni ya wanamgambo na kugundua takriban vituo 200 vya kurusha roketi, jeshi hilo lilisema.
Mashambulizi ya usiku kucha pia yalipiga mifumo ya kurushia roketi ya kuharibu vifaru huko kusini mwa Lebanon, ikiwa ni shambulizi la hivi karibuni zaidi kwenye mapigano ya mpakani ambayo yameongeza hofu ya kusambaa kwa mgogoro huo katika kanda.
Huko Uswiss, waziri mkuu wa Qatar alielezea haja ya kupatikana kwa suluhisho la mataifa mawili ili kufikia ufumbuzi wa kudumu, wakati akieleza tishio la kusambaa kwa mgogoro huo.
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani alisema wakati wa Kongamano la Uchumi huko Davos kuwa mashambulizi ya kijeshi hayata dhibiti mashambulizi dhidi ya meli kwenye Bahari ya Sham yanayofanywa na waasi wa Kihouthi huko Yemen, na badala yake kuna haja ya kujikita katika kutatua suala la msingi la vita huko Gaza
“Kilichoko sasa katika kanda ni kichocheo cha kuenea kwa vita,” Sheikh Mohammed alisema.
Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.