Vikosi vya Israel vilifanya mashambulizi mapya ya anga kote Ukanda wa Gaza, wakati wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza imesema Jumatatu kuwa mashambulizi ya Israel yaliwaua zaidi ya watu 130 siku moja iliyopita.
Jeshi la Israel limesema Jumatatu kuwa operesheni zake ni pamoja na kuwaua wanamgambo watano kaskazini mwa Gaza “ambao walikuwa wakijaribu kupata silaha,” pamoja na mashambulizi ya anga na ardhini ambayo yaliharibu ghala za kuhifadhi silaha katika eneo la Khan Younis kusini mwa Gaza.
Wizara ya afya ya Gaza, ambayo haitofautishi kati ya wapiganaji na raia katika idadi ya watu waliouawa, imesema Jumatatu kuwa idadi ya waliokufa kutokana na kampeni ya kijeshi ya Israel imeongezeka hadi 24,100 huku wengine zaidi ya 60,000 wakijeruhiwa.
Israel ilianza kampeni yake ya kijeshi ya kuliangamiza kundi la Hamas baada ya wapiganaji wa Hamas kuvuka mpaka na kuingia kusini mwa Israel, Oktoba 7 na kuwaua watu 1,200 na kuwateka nyara watu 240 katika shambulio hilo la kigaidi.
Forum