Jeshi la Israel lilisema Jumatatu operesheni zake zilihusisha kuwaua wanamgambo watano huko kaskazini mwa Gaza “waliokuwa wakijaribu kufikia silaha,” pamoja na mashambulizi ya anga na ardhini ambayo yaliharibu ghala za kuhifadhi silaha huko kusini mwa Gaza katika eneo la Khan Younis.
Wizara ya afya ya Gaza, ambayo haitofautishi kati ya ya vifo vya wapiganaji na raia, ilisema Jumatatu kuwa idadi ya watu waliofariki kutokana na kampeni ya kijeshi imeongezeka kufikia kiasi cha watu 24,100 huku wengine zaidi ya 60,000 wamejeruhiwa.
Israel ilianza kampeni zake za kijeshi kuwatokomeza Hamas baada ya wapiganaji wa Hamas kuvuka na kuingia kusini mwa Israel Oktoba 7, na kuua watu 1,200 na kuwateka nyara watu 240 katika shambulizi la kigaidi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong ametoa wito wa “sitisho endelevu la mapigano” huko Gaza wakati akiwa mwanadiplomasia hivi karibuni kuzuru eneo hilo kujadili mgogoro huo na juhudi za misaada ya kibanadamu.
“Hakuna sitisho la mapigano la upande mmoja na hakuna sitisho la mapigano linaloweza kuwepo bila masharti,” Wong alisema katika mkutano wake na waandishi wa habari kabla ya kuondoka kuanza ziara yake ambayo itamchukua hadi Jordan, Israel, Ukingo wa Magharibi na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.
Forum