Maafisa wa hospitali na walioshuhudia mashambulizi hayo walisema kuwa watu wasiopungua wanane, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa katika mashambulizi hayo.
Shirika la Associated Press limeripoti mashambulizi hayo yamepiga katika makazi ya raia huko Rafah na jengo la shule katikati ya mji wa Zuwaida.
Mashambulizi hayo yamefanyika saa kadhaa baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kukosoa vikali kuhusu kampeni ya kijeshi, ambayo imeuwa zaidi ya Wapalestina 27,000, kulingana na maafisa wa afya huko Gaza.
“Kwa maoni yangu, kama unavyojua, kuhusu mwenendo wa kujibu mashambulizi huko Gaza, na Ukanda wa Gaza, imepitiliza kiasi,” Biden alisema kujibu swali la mwandishi Alhamisi jioni huko White House.
Biden alisema amekuwa “akishinikiza kwa nguvu zote” kuwepo sitisho la muda la mapigano kwa ajili ya kutoa fursa ya kuachiliwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israeli. Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu ameukataa mpango huo, akiita mapendekezo ya Hamas “ni sawa na ndoto".
“Nimekuwa nikifanya juhudi bila ya kuchoka katika makubaliano hayo,” Biden alisema, akiongeza kuwa anaamini yanaweza kupelekea kufikia “hatua endelevu ya kusitishwa mapigano.”
Amesema amekuwa akishinikiza kuongezwa kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza.
“Kama unavyojua, hapo awali, rais wa Mexico, Sissi, hakutaka kufungua milango ili misaada ya kibinadamu iweze kuingia,” Biden alisema, akiwa anamkusudia Rais wa Misri Abdel-Fattah el-Sissi. “Niliongea naye. Nilimshawishi kufungua mpaka. Na kuongea na Bibi [Netanyahu] kufungua mpaka upande wa Israeli.”
Biden alisema hili wakati akitoa kwa haraka maoni kama ilivyopangwa ajibu ripoti ya mwendesha mashtaka maalum iliyotolewa Alhamisi.
Ripoti hiyo imehitimisha kuwa kwa makusudi alishikilia na kutoa taarifa za siri za kijeshi na usalama wa taifa na kugusia mapungufu ya kumbukumbu yake – kitu chenye kuwatia wasiwasi wapiga kura wa Marekani kabla ya uchaguzi wa rais mwezi Novemba.
Thuluthi tatu ya wapiga kura, ikiwemo nusu ya Wademokratik, wanasema wana wasiwasi kuhusu afya ya akili na mwili ya Biden, kulingana na utafiti wa maoni ulofanywa na shirika la habari la NBC ulotolewa mapema wiki hii.
“Kumbukumbu yangu iko vizuri,” Biden alisema.