Israel, Hamas wapambana, juhudi za wasuluhishi kusitisha mapigano zaendelea

  • VOA News

John Kirby

Israel ilisema Alhamisi majeshi yake yamepambana na wanamgambo wa Hamas kote Ukanda wa Gaza, wakiwaua darzeni ya wapiganaji eneo la kati na kaskazini mwa ukanda huo.

Mapigano yaliendelea wakati wasuluhishi wa pendekezo jipya la kusitishwa mapigano wakisubiri kusikia maendeleo yaliyofikiwa katika makubaliano kati ya Israel na Hamas ambayo yatapelekea kusitishwa mapigano kwa muda mfupi na kuachiwa kwa wafungwa wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza.

Muongozo huo wa pendekezo umetokana na mazungumzo ya Paris yaliyofanyika kati ya maafisa wa Marekani, Israel, Qatar na Misri mapema wiki hii. Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh alikuwa anatarajiwa kusafiri kwenda Cairo kujadili mpango huo.

Ismail Haniyeh

Alipoulizwa kuhusu maelezo ya pendekezo hilo wakati akitoa muhtasari Jumatano huko White House, msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa John Kirby alisema hakuna vipengele vilivyokamilika mpaka pale makubaliano yatapokamilishwa.

“Nitakwambia kuwa, kwa hatua zaidi, tunatazamia kuwepo sitisho la mapigano la muda mrefu ndio lengo,” Kirby aliwaambia waandishi wa habari. “Ni kwa muda gani? Hiyo yote ni sehemu ya majadiliano, lakini itakuwa muda mrefu zaidi kuliko tulivyoshuhudia mwezi Novemba, ambayo ilikuwa ni kiasi cha wiki moja.”

Zaidi ya mateka 100 waliokuwa wamechukuliwa na Hamas wakati wa shambulizi la kigaidi la Oktoba 7 ndani ya Israel waliachiliwa wakati wa sitisho la mapigano mwezi Novemba na kubadilishana na Wapalestina 240 waliokuwa wamefungwa na Israel. Inaaminika kuwa Hamas bado wanawashikilia mateka wengine 100 au karibu na idadi hiyo.

Kirby alisema kuwa inawezekana kuachiliwa mateka wengi zaidi kutoka Gaza iwapo kutakuwa na sitisho la mapigano la muda mrefu, na kuwa sitisho la muda mrefu litawezesha kuongezeka kuingia kwa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia wa Gaza.

“Tunataka kuona kuwa makubaliano haya yanafikiwa,” Kirby alisema. “Tunataka kuona yamefikiwa haraka iwezekanavyo.”

Hamas imetaka sitisho la la kudumu la mapigano na majeshi ya Israeli yaondoke kabisa kutoka Gaza.

Israel iliapa kuiangamiza Hamas, ambayo inatawala Gaza na imewekwa katika orodha ya taasisi za kigaidi na mataifa ya Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine.

Israel ilianzisha mashambulizi ndani ya Gaza mara baada ya Hamas kufanya shambulizi lililouwa takriban watu 1,200, wengi wao raia, kulingana na hesabu zilizojumuishwa na Israeli.

Wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza inasema idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel imefikia watu 26,900.

Baadhi ya taarifa katika ripoti hii imetolewa na mashirika ya habari ya AP, AFP na Reuters.