Mashirika ya kutetea haki za binadamu yameishutumu Tehran kwa kuongezeka utoaji wa adhabu ya kifo kueneza hofu katika jamii kutokana na vuguvugu la maandamano lililozuka Septemba mwaka jana, kutokana na kifo cha Mahsa Amini, ambaye alikuwa amekamatwa kwa madai ya kukiuka sheria kali za mavazi kwa wanawake.
Shirika la Haki za Kibinadamu la Iran lenye makao yake makuu nchini Norway lilisema, idadi hiyo ya watu 354, kwa miezi sita ya kwanza, hadi Juni 30, ilikuwa asilimia 36 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022, ambapo watu 261 waliuawa.
Ikisisitiza wasiwasi kwamba makabila yasiyo ya uajemi yameathiriwa kupita kiasi kutokana na kunyongwa kwa watu nchini Iran, ripoti hiyo ilieleza kwamba asilimia 20 ya hukumu zote za kunyongwa ni za walio wachache wa kabila la Sunni Baluch.
Ilisema watu 206 walinyongwa kwa mashtaka yanayohusiana na dawa za kulevya, ambalo ni ongezeko la asilimia 126, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Wanawake sita walikuwa miongoni mwa walionyongwa katika kipindi hicho, huku wanaume wawili wakinyongwa hadharani, iliongeza ripoti hiyo.