Mamlaka nchini Haiti zilitumia mitandao ya jamii kuwatahadharisha wananchi wake juu ya kimbunga, wakiwasihi wale wanaoishi karibu na maji au milimani kuondoka.
Kituo cha Taifa cha Kimbunga huko Miami kimesema kimbunga daraja la kwanza kimeonekana takriban kilomita 635 mashariki -kusini mashariki mwa Isla Beata, Jamhuri ya Dominican, na kilikuwa kinaelekea magharibi – kaskazini magharibi kwa kasi ya kilomita 48 kwa saa na upepo wenye nguvu ya juu ya kilomita 140 kwa saa.
Kimbunga Elsa kinatarajiwa kupungua kasi na kuwa dhoruba ya tropiki baada ya kutua Cuba, na utabiri wa muda mrefu wa kituo cha Kimbunga unaonyesha kwamba kinapungua kasi na kitawasili Florida kikiwa na dhoruba ya kawaida. Lakini aina nyingine za utabiri, hata hivyo zinaonyesha kuwa kimbunga hicho kitafika Ghuba au kwenye pwani ya Atlantic.
Maonyo ya kimbunga yametolewa Jumamosi kwa pwani ya kusini ya Jamhuri ya Dominican kuanzia Punta Palenque hadi kwenye mpaka wake na Haiti ; sehemu ya kusini mwa Haiti kuanzia Port Au Prince hadi mpaka wa kusini na Jamhuri ya Dominican; na Jamaica kuanzia Jumapili.
Ufuatiliaji wa kimbunga unaendelea katika majimbo ya Cuba ya Camaguey, Granma, Guantanamo, Holguin, Las Tunas, na Santiago de Cuba
Vyanzo vya habari : VOA News, Associated Press na Reuters.