Hofu ya Kirusi Corona : Kenya Airways, RwandaAir zasitisha safari za China

Ndege za Kenya Airways zikiwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi, Kenya, April 28, 2016.

Mashirika ya ndege ya Kenya Airways na RwandaAir mapema leo yametangaza kusitisha safari zote za ndege kuelekea na kutoka China baada ya kirusi hicho kuenea kwenye karibu mataifa mengine 18.

Kirusi corona kimesababisha vifo 213 nchini China na maambukizi kwenye mataifa mengine.

Nchini Kenya, siku ya Jumanne, mwanafunzi aliwekwa kwenye karantini katika hospitali mjini Nairobi, baada ya kuwasili kutoka Wuhan, China, eneo ambalo ndio chimbuko la mlipuko huo.

Vyanzo vya habari vimesema Kenya Airways imesema kuwa bado iko kwenye mazungumzo na wizara ya afya na wizara ya mambo ya nje juu ya wakati muafaka wa kusitisha safari kwenda China.

Hata hivyo Kenya imesema safari za mji mkuu wa Thailand, Bangkok zinaendelea kama kawaida.

Marekani imeonya raia wake kutosafiri hadi China wakati idadi ya vifo kutokana na virusi vya corona, huku Shirika la Afya Duniani, WHO, Alhamisi likitangaza mlipuko huo kuwa dharura ya kiafya inayohitaji hatua za kimataifa.

Shirika hilo limesema wasi wasi mkubwa ni kutokana na maambukizi kutoka binadamu mmoja hadi mwingine, wakati serikali ya China ikisema kuwa idadi ya kesi za maambukizi zilizodhibitishwa nchini humo imefikia 9,600.

Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amepongeza China kutokana na hatua ilizochukua akiongeza kuwa shirika lake halijapendekeza hatua dhidi ya usafiri au biashara na China.

Tedros Adhanom amesema : "Natangaza dharura ya kimataifa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona. Sababu kubwa ya tangazo hili siyo mambo yanayoendelea China bali ni maambukizi yaliotangazwa kwenye mataifa mengine."

"Wasi wasi mkubwa ulioko ni kuenea kwa kurusi hicho kwenye mataifa yasiyo na uwezo mkubwa wa kudhibiti hali, au ambayo hayapo tayari kukabiliana na janga hilo. Hili naliweka wazi kwamba hatua hii hailengi kutokuwa na Imani na China."

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.