Hayati Magufuli aagwa na marais tisa wa Afrika

Jeneza la hayati John Pombe Magufuli likiwa linaagwa kitaifa mjini Dodoma. Picha na Ikulu.

Marais wa nchi tisa za Afrika ni miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria shughuli ya kitaifa ya kumuaga aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati, John Pombe Magufuli jijini Dodoma Jumatatu. 

Hayati Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka 2021 jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya moyo, tayari ameagwa jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kabla ya mwili wake kupelekwa Dodoma kwa ajili ya shughuli hiyo ya kitaifa.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amewahakikishia Watanzania kuendeleza umoja na mshikamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki huku pia akiahidi kuendelea kufanya kazi na Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amemlilia hayati John Magufuli kama mwana wa Afrika aliejitoa kuona bara hili linakombolewa kiuchumi.

Marais wengine waliohudhuria kuagwa kwa Hayati John Magufuli ni pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, rais wa Afrika Kusini, Rais wa Botswana, Rais wa Muungano wa visiwa vya Comoro, Rais wa Malawi, Rais wa Zambia na Rais wa Zimbabwe pamoja wa wawakilishi wa nchi nyingine za ndani na nje ya Afrika.

Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asubuhi pia walipata wasaa wa kipekee wa kumuaga hayati John Pombe Magufuli katika viwanja vya bunge jijini Dodoma.

Magufuli anatarajiwa kuzikwa Ijumaa wiki hii Wilayani Chato, mkoani Geita. Kesho wananchi wa Zanzibar watapata fursa ya kumuaga hayati Magufuli katika uwanja wa Amani, visiwani Unguja.

Wakati huohuo Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametangaza akiwa mjini Dodoma kwamba Jumatatu Machi 22 ni siku ya kitaifa kwa ajili ya shughuli za kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa hayati John Pombe Magufuli.

Marais tisa kutoka mataifa mbali mbali barani Afrika, pamoja na wananchi wameongozwa na Rais Samia Hassan Suluhu wa Tanzania katika kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Dodoma.

Hayati Magufuli alifariki Machi 17 katika hospitali ya Mzena huko Dar es Salaam mahala ambako alilazwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa moyo. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika Machi 26 nyumbani kwao Chato katika mkoa wa Geita.